2014-07-23 12:19:39

Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu, ili amani iweze kutawala tena!


Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, imekuwa ni fursa kwa Waamini wa dini ya Kiislam kujikita zaidi na zaidi katika Swala, Mfungo pamoja na kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha.

Ni muda ambao umewawezesha waamini wa dini ya Kiislam kujenga na kuimarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani. Siku kuu ya Id Al Fitri ni wakati wa kutakiana kheri na mema kwa kujielekeza zaidi katika masuala ya kisayansi, haki, ibada, huduma, huruma, ushauri, kutafuta mema na kuachana na mabaya. Waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kufanya tafakari ya kina kuhusu changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, yaani: athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na kiu ya haki na amani miongoni mwa mataifa.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa matashi mema kutoka kwa Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam wanaoishi ndani na nje ya Jimbo kuu la Torino katika maadhimisho ya Siku kuu ya Id Al Fitri, inayokuja kila baada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa waamini wa dini ya Kiislam.

Askofu mkuu Nosiglia anasema, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimepelekea ukosefu wa fursa za ajira kwa mamillioni ya watu, lakini zaidi miongoni mwa vijana kiasi kwamba, wengi wao wamechanganyikiwa na kukata tamaa ya maisha, changamoto kwa Serikali na watunga sera kuhakikisha kwamba, wanaibua mbinu mkakati utakaosaidia kutoa fursa za ajira kwa vijana ili waweze kuwa na matumaini ya maisha yaliyo bora na tayari kuzisaidia familia zao.

Ikumbmukwe kwamba, waamini wana utajiri mkubwa ndani mwao ambao unaweza kutumika katika ujenzi wa misingi ya haki, mafao ya wengi, udugu na mshikamano kati ya watu pamoja na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Askofu mkuu Nosiglia anasema kwamba, watu wana kiu ya haki na amani ya kudumu, lakini matumaini ya amani yanaonekana kana kwamba, yanazidi kutoweka na badala yake mtutu wa bunduki unazidi kushika kasi ya ajabu, kiasi cha kuwaacha watu wakiwa wameshika tama na kujiuliza kuhusu juhudi za Baba Mtakatifu Francisko za kuwakutanisha Marais wa Israeli na Palestina mjini Vatican hapo tarehe 8 Juni 2014, zimetoweka na kufutika kama ndoto ya mchana?

Baba Mtakatifu Francisko alikumbushia kwamba, vita na mtutu wa bunduki kamwe havitaweza kuleta suluhu ya haki na amani, bali amani ya kweli inajengeka katika msingi wa majadiliano, toba na wongofu wa ndani; kwa kukazia mafao ya wengi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu. Ikumbukwe kwamba, ujenzi wa amani unahitaji ujasiri wa ajabu kwani ni rahisi sana kuanzisha na kuendeleza vita. Kumbe, kuna haja ya kuondokana na kishawishi cha kuendeleza chuki na uhasama kati ya watu pamoja na kuendelea kutegemea ulinzi na tunza kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuthaminiana kama "ndugu".

Askofu mkuu Cesare Nosiglia anasema, hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Ni matumaini yake kwamba, matunda ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani utawawezesha waamini wa dini ya Kiislam, kujikita zaidi katika kutafuta na kudumisha haki na amani kati ya watu. Waamini wa dini zote, wapendane na kuheshimiana kama ndugu, kwa kukuza na kuendeleza msamaha pamoja na kukataa katu katu kishawishi cha matumizi ya nguvu. Ni pale tu waamini wote watakapotoa kipaumbele cha kwanza kwa ujenzi wa amani, hapo ndipo kweli Mwenyezi Mungu atapata utukufu na amani kutawala!







All the contents on this site are copyrighted ©.