2014-07-23 11:37:03

Kozi maalum za kudhibiti migogoro kuanza kutolewa na Chuo Kikuu cha ECUSTA


Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, kilichoko nchini Ethiopia, ECUSTA, ni utekelezaji wa wazo lililotolewa na Hayati Meles Zenawi, aliyekuwa Waziri mkuu wa Ethiopia wakati alipomtembelea Mtakatifu Yohane Paulo II mjini Vatican. Kwa siku za usoni, Chuo hiki kitajielekeza zaidi katika kutoa mafunzo ya haki na amani, ili kuzijengea uwezo nchi za AMECEA katika kupambana na kudhibiti migogoro na kinzani za kijamii, kisiasa na kimaadili.

Hiki ni Chuo Kikuu ambacho ni kinara katika utoaji wa huduma ya elimu nchini Ethiopia na kwamba, ni sehemu ya Familia ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Nchi za AMECEA. Ni mchango uliotolewa na Padre Hagos Hayish, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA unaoendelea mjini Lilongwe, Malawi.

Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Ethiopia, kinatarajiwa kuanza kutoa kozi maalum kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya haki na amani kwa nchi za AMECEA kama sehemu ya mchakato wake wa maboresho katika huduma za kijamii zinazotolewa Chuoni hapo. Serikali ya Ethiopia inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na ECUSTA kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ethiopia na kwamba, Serikali imekwisha toa kiasi cha ekari sitini za ardhi kwa ajili ya mchakato wa upanuzi wa Chuo hiki.

Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, kilianzishwa katika eneo ambalo hapo zamani lilikuwa ni Chuo Kikuu cha Ethiopia na kwamba, kwa sasa ECUSTA kinazidi kuchanja mbuga katika sekta ya elimu nchini Ethiopia kwa kuwa ni kati ya taasisi kubwa zinazotoa elimu ya juu nchini humo.

Wakati huo huo, Dr. Mary Shawa, katibu mkuu wa Wizara ya Jinsia, Watoto, Walemavu na Jamii nchini Malawi, amewataka Wanawake Wakatoliki kutoka katika nchi za AMECEA kuhakikisha kwamba, wanatumia mitandao ya kijamii inayomilikiwa na kuendeshwa na AMECEA ili kushirikisha vipaumbele na ajenda za maendeleo: kijamii na kiuchumi.

Dr. Shawa anasema kwamba, AMECEA linaweza kuwa ni jukwa la maendeleo endelevu kwa wanawake kutoka AMECEA, ikiwa kama kweli wanataka kuwa wajasiriamali watakaochangia katika mchakato wa maendeleo ya familia zao. Ni kwa njia ya mikopo na misaada inayotolewa na AMECEA, leo hii kuna wanawake wengi ambao wamejikomboa kiuchumi na kwa sasa ni wawekezaji wakuu katika sekta ya uchumi na maisha ya kijamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.