Vingozi wa kidini nchini Uingereza wametoa tamko la pamoja kupinga muswada wa sheria
unaotaka kuhalalisha mchakato wa kifo laini kwa kuwapatia msaada wa kitabibu wale
wanaotaka kujinyonga, muswada ambao umeanza kujadiliwa nchini Uingereza.
Muswada huu
unampatia uwezo wa kisheria daktari kutoa dawa itakayochochea kifo pole pole kwa wagonjwa
wa muda mrefu au wale ambao wana magonjwa yasiyokuwa na tiba. Moja ya masharti ni
kwamba, mgonjwa anapaswa kufanya maamuzi haya magumu kwa utashi kamili pasi na shuruti.
Viongozi
wa kidini wanasema, maisha ya mwanadamu ni zawadi na tunu kubwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, kumbe inapaswa: kupendwa, kulindwa na kuendelezwa. Huu ndio msingi thabiti
wa sheria unaoweza kudumisha mahusiano mema katika jamii. Muswada wa sheria unaonesha
mwelekeo tenge wa Jamii inayotakiwa nchini Uingereza, kwa kutozingatia uhai wa mwanadamu
na kwamba, utu na heshima ya mtu inapimwa kutokana na mchango wake katika Jamii. Lakini
kila mtu anapaswa kupendwa, kusaidiwa na kulindwa hata kama wakati mwingine mtu kama
huyu anashindwa kujipenda na kujilinda mwenyewe.
Viongozi wa kidini nchini
Uingereza wanasema kwa dhati kwamba muswada wa sheria unaojadiliwa nchini Uingereza
kwa sasa una lengo la kumong’onyoa tunu msingi za maisha kwa siku za usoni, kiasi
cha kushindwa kuheshimu na kuwalinda watu wake. Shauku ya mtu kutaka kukatisha maisha
yake binafsi inaweza kuchangiwa na mambo mengi kutoka ndani na nje ya mtu husika.
Muswada wa sheria utawatendea wanyonge na wagonjwa wa mgonjwa yasiokuwa na tiba, watu
ambao wanapaswa kupendwa na kusaidiwa, lakini Jamii inawageuzia kisogo.
Viongozi
wa kidini nchini Uingereza wanasema, kinachotakiwa hapa ni tiba makini kwa ajili ya
wagonjwa walioko kufani pamoja na kuendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa ndugu
na jamaa wanaowauguza wagonjwa hawa, jambo ambalo linaonesha Jamii inayowajali watu
wake na huko ndiko ambako Jamii inapaswa kuelekeza nguvu zake. Wagonjwa wanapaswa
kuhudumiwa na wala si kusukumizwa kwenye tanuru la kifo. Dhamana ya maisha ya mtu
iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake.