2014-07-22 14:53:31

Mshikamano wa Papa na wananchi wa Iraq


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 20 Julai 2014 alipiga simu na kuzungumza na Patriaki Ignatius Youssef Younan wa III wa Kanisa Katoliki la Siro, Antiokia, kuonesha mshikamano wake wa kiroho na Wakristo pamoja na raia wasiokuwa na hatia wanaoendelea kuteseka nchini Iraq, hasa mjini Mosul ambako vita inazidi kupamba moto!

Taarifa zinaonesha kwamba, mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Ignatius yamedumu kwa takribani dakika tisa na kwamba, Patriaki amemshukuru sana Baba Mtakatifu kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi wa Iraq. Baba Mtakatifu anawaomba wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza nguvu kusitisha vita hii ambayo inaonekana kuwa na mlengo wa madhulumu ya kidini zaidi.

Baba Mtakatifu anasikitishwa na ukimya unaoneshwa na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na mauaji yanayoendelea huko. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea waamini na wananchi wote wa Iraq ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha. Wakristo eneo la Mosul wanazidi kutoweka baada ya kukaa katika eneo hili kwa kipindi cha zaidi ya miaka elfu mbili. Baadhi yao wamekimbilia kutafuta hifadhi ya kisiasa huko Kurdstan.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, tarehe 19 Julai 2014 alikutana na kuzungumza na Patriaki Younan mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.