2014-07-22 11:11:38

Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi laonja joto la AMECEA!


Jumapili iliyopita, Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi liligubikwa na shamrashamra za maadhimisho ya Ibada za Misa Takatifu zilizoongozwa na Maaskofu wa AMECEA katika Parokia mbali mbali, Jimboni humo, huku wakiwa wamesindikizwa na wajumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi.

Katika Parokia ya Mtakatifu Francis, Kanengo, Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na mahubiri kutolewa na Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha.

Amewakumbusha waamini wa Jimbo kuu la Lilongwe, Malawi kwamba, Yesu Kristo Mfufuka anaendelea kutenda kazi zake ndani ya Kanisa na ndiyo maana AMECEA imeamua kuimarisha maisha na utume wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kama sehemu ya mikakati yake ya Uinjilishaji Mpya. Mara baada ya Misa, Ujumbe kutoka Tanzania ulitembelea miradi mbali mbali ya maendeleo inayosimamiwa na Shirika la Wamissionari wa Afrika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Malawi.

Ujumbe wa Maaskofu Katoliki Uganda, uliadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Afrika, Maula. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu John Baptist Odama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda alikazia umuhimu wa kujenga na kudumisha mchakato wa upendo na mshikamano, vinginevyo wanaweza kujikuta wamemezwa na malimwengu na kutawaliwa tena na upagani.

Ujumbe wa Maaskofu kutoka Sudan ya Kusini, umeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Utatu Mtakatifu, Kawale na Ibada kuongozwa na Askofu msaidizi Santo Loku Pio wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini. Wao mara baada ya misa walitembelea miradi mbali mbali inayoendeshwa Parokiani hapo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia, likiongozwa na Askofu mkuu Berhaneyesus Souraphiel, amewashukuru wananchi wa Malawi kwa wema na ukarimu wao na kwamba, vijana wa AMECEA wanapaswa kufundishwa tunu hizi msingi katika maisha yao badala ya kushikwa na kishawishi cha kutaka kukimbilia ughaibuni ili kutafuta malisho bora zaidi, lakini huko wengi wao wanakumbana na majanga. Wakristo wajenge na kuoneshana upendo na huruma pamoja na kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, upendo na mshikamano wa kitaifa. Maaskofu Katoliki wa Ethiopia wameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Parokia ya Don Bosko.

Wajumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea, Djibout na Somalia waliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Yohane, Msamba na hapa wamewashirikisha waamini Parokiani hapo mang'amuzi yao ya maisha ya Kikristo.

Wajumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia, wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mtima Woyera. Askofu mkuu Telesphore Mpundu ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu na mahubiri kutolewa na Askofu Benjamin Phiri, aliyewataka waamini kushikamana na Yesu katika maisha yao na kuachana kabisa na mtindo wa maisha ya undumilakuwili, kwa kumpatia nafasi Shetani ili aweze kuwapepeta kama ngano!

Kardinali Jonh Njue na ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ameongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Parokia ya Mtakatifu Kizito. Kardinali Njue amewataka waamini kucharuka katika maisha yao kwa kuonesha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini wahudhurie na kushiriki kikamilifu maisha na utume wa Kanisa pamoja na kupokea Sakramenti za Kanisa.

Waamini wajitahidi kuonesha maisha adili na matakatifu, changamoto kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Kutokana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza Barani Afrika kuna haja kwa Kanisa kujielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya kwa kujitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika uhalisia wa maisha ya waamini.







All the contents on this site are copyrighted ©.