2014-07-22 15:13:39

Balozi wa Vatican nchini Angola asikitishwa na Serikali kuchelewa kutoa kibali cha kurusha matangazo kwa Radio Ecclesia!


Askofu mkuu Novatus Rugambwa, Balozi wa Vatican nchini Angola ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na Serikali ya Angola kuchelewesha kutoa ruhusa kwa Radio Ecclesia kuongeza nguvu ya matangazo yake ili yaweze kusikika nchi nzima. Hadi wakati huu, matangazo ya Radio Ecclesia yasikika mjini Luanda, Angola peke yake, ingawa ni Radio ya siku nyingi iliyoanzishwa kunako mwaka 1954.

Radio hii katika uhai wake imekumbana na misukosuko mingi kiasi hata cha kufungiwa kurusha matangazo yake na Serikali ya MPLA, baada ya Angola kujitwalia uhuru wake. Radio Ecclesia ni kati ya njia muhimu sana za mawasiliano nchini Angola na kwa kipindi cha miaka mingi imeomba ruhusa ya kupata kibali cha kurusha matangazo yake nchi nzima lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote.

Askofu mkuu Novatus Rugambwa anasema, watu wana kiu ya kusikiliza matangazo yanayorushwa na Radio Ecclesia, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaokwenda sanjari na matumizi ya njia za kisasa za mawasiliano ya jamii. Askofu mkuu Rugambwa ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anahojiwa na Radio Saut ya Ujerumani alipokuwa anatembelea Jimbo Katoliki la Benguela.

Kwa mara ya kwanza Askofu mkuu Rugambwa tangu aanze utume wake nchini Angola kunako mwaka 2010 ameonesha masikitiko haya makubwa. Itakumbukwa kwamba, kwa sasa kuna mkutano unaoendelea mjini Luanda kwa nchi zile zinazozungumza Kireno na kwa mara ya kwanza mkutano huu unafanyika nchini Angola.







All the contents on this site are copyrighted ©.