2014-07-21 08:05:03

Maisha Mchanganyiko ya Kijamii- Mhamiaji- Sehemu ya kwanza


Baada ya kuzungumzia Wakimbizi katika maisha mchanganyiko ya kijamii, leo na tutazame kundi jingine la watu, nao ni Wahamiaji, kundi ambalo uwepo wake si rahisi kukwepeka katika maisha ya kawaida ya kijamii, hasa katika ulimwengu wa leo wa utandawazi.
Uhamiaji wa binadamu ni harakati na watu kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa nia ya kutaka kuwa na maisha tulivu zaidi katika eneo jipya. Kwa kawaida mtu anayeitwa mhamiaji ni yule anayetoka umbali mrefu, au kutoka nchi moja hadi nyingine, au bara hadi bara, lakini pia kuna uhamiaji wa ndani ya nchi. Uhamiaji unaweza kuwa , mtu binafsi, familia au muungano wa familia na hata makundi makubwa, ilivyo historia nyingi za wakulima na wafungaji , wanaohama kutoka eneo moja hadi jingine, kutoka wilaya hadi wilaya au mkoa hadi mkoa, nchi hadi nchi. Aidha kulingana na mazingira ya kihistoria, hali na mtazamo, pia kuna wahamiaji wanaoitwa kama walowezi, kama walivyo walowezi Wazungu Afrika Kusini. Wote hao, huwa na sifa moja kuu, hamu ya kuhamia eneo jipya kwa lengo la kutafuta maisha yaliyo bora zaidi.
Katika utambuzi kwamba, moyo wa binadamu umeumbwa na hamu ya kutaka kupata mengi zaidi, ufahamu, elimu, mali, maisha, miliki, mamlaka na kadhalika, hupata msukumo mkali wa ndani, kwenda kutafuta hayo. Na ndivyo ilivyokuwa tangu zama za kale, hata kwa wale wanaoitwa wavumbuzi, kama Christopher Columbus, Marco Polo , Newton, n.k, walifunga safari za mbali kwenda kutafuta yanayofaa zaidi katika maisha. Na pia ndivyo kwa wanasayansi, wanatafuta kuboresha maisha , kama ilivyo dhahiri leo hii kwamba, mtu hushinda Afrika na kupata kifungua kinywa chake barani Ulaya. Hulala China na kuamka Marekani! Ulimwengu ambamo sasa watu wanashirikishana soga kama vile wako chumba kimoja, na kumbe wanatenganishwa na umbali wa maelfu ya kilomita. Kwa hakika haya ni maendeleo ya kasi.
Ni katika hamu hiyo asili ya binadamu, kuyatafuta maisha yaliyo bora zaidi, ambamo mna matokeo ya kutaka kuyahama matatizo na kwenda mahali penye ahueni kimaisha. Hamu ya kuboresha maisha inayo usukuma moyo wa mtu kuhama , iwe kwa wale wanaohama kutoka Ulaya kwenda Afrika au wanaotoka Afrika kwenda Ulaya . Wote nia yao kuu ni kutafuta mahali wanapoweza kufanikisha maisha bora zaidi, kuliko wakibaki katika maeneo yao asilia.
Katika hali hiyo, mhamiaji basi ni nani. Na kuna manufaa yoyote ya kuwa mhamiaji? Na tunazama katika mada hii kwa kurejea ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisco alio utoa kwa ajili ya Wahamiaji na Wakimbizi kwa mwaka 2014. Ujumbe aliouandika chini ya Jina : Wahamiaji na Wakimbizi: Kuelekea Dunia iliyo bora zaidi.
Baba Mtakatifu Francisco, katika ujumbe huo, ameyatafakari mapito ya kijamii katika nyakati hizi akisema kwamba, katika njia zisizo za kawaida, Jamii ya binadamu sasa inapita katika mchakato wa kutegemeana pamoja na mwingiliano usiokuwa wa kawaida katika ngazi zote hata kimataifa. Na hivyo ni wakati ambamo hakuwezi kukosa changamoto na matatizo, hasa katika taratibu zinazolenga kuboresha hali ya maisha ya familia ya binadamu, si tu kiuchumi, lakini pia kisiasa na kiutamaduni sawia.
Ujumbe wa Papa unatahadharisha kwamba, cha msingi katika maisha haya mchanganyiko, ni kukumbuka kwamba, kila mtu ni sehemu ya ubinadamu na ni mmoja wa familia nzima ya watu na matumaini yote ya maisha bora ya baadaye. Kwa hisia hizo , Baba Mtakatifu Francisco ameeleza , ndizo zilimsukuma kuchagua mada ya Wahamiaji na wakimbizi, kulekea dunia iliyo bora zaidi, isindikize mwaka huu katika kuwapokea wahamiaji na wakimbizi.

Papa ameendelea kutazama kukua kwa wimbi la binadamu kuhama, akirejea maneno yaliyotolewa na mtangulizi wake, Papa Benedict XVI, kwamba hii ni “ishara ya nyakati" ( ujumbe kwa mwaka 2006 kwa Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani). Uhamiaji mara nyingi huashiria au kutangaza kushindwa au uwepo wa mapungufu ndani ya eneo , Nchi au jumuiya ya kimataifa katika kukomesha madhulumu dhidi ya ubinadamu . Lakini pia kwa upande mwingine, huonyesha hamu ya binadamu kufurahia umoja na mshikamano uliosimikwa katika mitazamo ya kuheshimu tofauti, kukubalika na ukarimu katika kushirikiana na mgawanyo sawa wa mali za hapa duniani, na kwa ulinzi na maendeleo ya hadhi na umuhimu wa kila binadamu.
Papa alifafanua kwa upande Ukristo, hali halisi ya uhamiaji, kama ilivyo katika hali halisi nyingine za haki za binadamu, huashiria mvutano kati ya uzuri wa viumbe, unaojionyesha katika neema ya ukombozi na fumbo la dhambi. Mshikamano, kukubalika, na ishara ya udugu na ufahamu wa uwepo huenda sambamba na kukataliwa, ubaguzi, biashara haramu na unyonyaji, mateso na kifo. Na hasa kinachosumbua ni zile hali ambamo uhamiaji unakuwa tena si jambo la hiari, lakini kama matokeo ya mashinikizo yaliyo nje ya ubinadamu. Mtu kulazimika kukimbia madhulumu mbalimbali ya utendaji haramu wa binadamu, kama kazi za sulubu, kutekwa nyara, na mateso ya mengine ya mwili yakiwemo mauaji na utumwa. Leo hii kazi za kutumikishwa katika hali ya utumwa limekuwa ni jambo la kusikika. Lakini pamoja na matatizo na hatari na hali ngumu zilizoko mbele yao, bado watu wanahama maeneo yao kwa wingi, wakiwa wamejawa na imani na tumaini thabiti, kwamba huko wanakokwenda wataweza kuwa na maisha bora ya baadaye, si tu kwa ajili yao wenyewe lakini kwa familia zao na wale walio karibu nao.
Ujumbe wa Papa Francisco unaendelea kututaka tujiulize nini hasa kinacho hitajika katika kujenga ulimwengu ulio bora zaidi kwa maisha? Je haipaswi kulenga katika maendeleo halisi na muhimu yenye kuheshimu ya maisha ya kila mtu, katika kutafuta majibu yanayo faa kukidhi mahitaji ya watu binafsi na familia, na kuhakikisha kwamba zawadi ya Mungu ya maisha inaheshimiwa, kulindwa na kudumishwa ? Papa Francisco alihoji na kurejea waraka wa Papa Paul VI, juu ya Maendeleo ya Watu, 6, ambamo ameeleza kuwa, matarajio ya watu leo hii, ni uhakika wa kupata chakula, tiba kwa magonjwa na ajira ya kuridhisha , kama utendaji zaidi katika uwajibikaji binafsi, kutenda zaidi, na kujifunza zaidi, na kuwa na mali na maisha bora zaidi .

Moyo wa binadamu una hamu ya kutenda zaidi na zaidi, kupata maarifa na zaidi au mali zaidi na zaidi n.k. Lakini maendeleo hayawezi kuwa ya ukuaji wa uchumi peke yake , bali pia ni muhimu kuzingatia hoja zingine katika ubinadamu na mwelekeo wa mtu, ikiwa ni pamoja mambo ya kiroho. Mapapa wote wanasisitiza , asiwepo mtu wa kupuuzwa, licha ya hali yake ya umaskini, ugonjwa, kufungwa, au kuwa mgeni, au mhamiaji au mkimbizi (cf. Mt 25:31-46). Na hili linaweza kufanikishwa kwa kuachana na utamaduni wa ulafi na ubinafsi wa kujilimbikizia , bali kwa kujenga utamaduni wa umoja na mshikamano katika kugawana na kushirikishana utajiri wa dunia na kuwakubali wengine.
Baba Mtakatifu Francisko anaonya , kwa mtazamo huo, Mhamiaji hapaswi kuchezewa kama kete katika bao. Wahamiaji ni watu wa kawaida ambao, kwa msukumo asilia wa ndani ya moyo na kwa sababu mbalimbali , huamua kuondoka katika maeneo yao na kwenda sehemu nyingine kujaribu kuboresha maisha si kwa ajili yao tu lakini pia kwa familia zao na jamii zao.
Leo hii takwimu za Idadi ya watu, wanaohama kutoka nchi hadi nchi au bara hadi bara jingine, au kuhama maeneo ndani ya nchi zao na maeneo ya kijiografia, ni kubwa pengine kuliko hata ilivyowahi kutokea kihistoria.
Kanisa tangu mwanzo wake , daima huambatana na wahamiaji katika safari yao, na hasa hupenda kuelewa chanzo cha uhamiaji, ili liweze kutenda vyema zaidi na kuondokana na madhara yake hasi, ila kuongeza ushawishi wake chanya kwa jamii asilia, walio katika kuhama na hatima ya safari yao.

Na hivyo, wakati maendeleo ya ulimwengu bora yanapohimizwa , Mama Kanisa, hawezi kukalia kimya kashfa ya umaskini katika hali zake zote, na hasa ikikuzwa na vurugu, unyonyaji, ubaguzi, vikwazo mbinu kwa uhuru wa kimsingi, iwe kwa mtu binafsi au kwa vikundi. Mara nyingi haya yameonekana kuwa sababu msingi zinazofanya uwepo wa wimbi la watu kuingia katika harakati za kuhamahama, ikionyesha uwepo wa uhusiano kati ya uhamiaji na umaskini. Waliokimbia kutoka hali ya umaskini uliokithiri au mateso kwa matumaini ya maisha bora ya baadaye, au tu ili kuokoa maisha yao wenyewe, kwa sababu hizo, mamilioni ya watu huchagua kuhamia maeneo mengine. Bahati mbaya pamoja na matumaini na matarajio yao, wao mara nyingi hupambana na kutoaminiwa, kukataliwa na kutengwa, na hata kunyimwa uhuru wa dhamiri na kupokonywa heshima ya ubinadamu wao.
Katika ukweli wake, Papa Francisco alisisitiza , uhamiaji leo hii, katika mtazamo mpana wa utandawazi, unahitaji mtazamo na mbinu mpya katika kusimamia, kulinda usawa kwa ufanisi zaidi , na hili linahitaji ushirikiano wa kimataifa, huruma kubwa.
Imeandaliwa nami T.J.Mhella.







All the contents on this site are copyrighted ©.