CRS kuendelea kushikamana na Nchi za AMECEA katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
Dr. Carolyn Woo, Mkurugenzi mtendaji na Rais wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki
Marekani, CRS, katika mkutano wa kumi na nane wa AMECEA anasema kwamba, ushuhuda
wa imani tendaji ni kati ya changamoto zinazopewa kipaumbele cha kwanza na Shirika
hili katika mipango na mikakati yake na kwamba, wanapania kuendeleza na kudumisha
mshikamano wa kidugu na AMECEA katika utekelezaji wa mikakati yake kama inavyofafanuliwa
kwa kina na mapana katika Waraka wa kichungaji, Dhamana ya Afrika, Africae Munus.
CRS inatambua changamoto zinazoikabili nchi za AMECEA, ikiwa ni pamoja na
kinzani za kidini, kisiasa, kijamii na kiuchumi; kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini,
majanga asilia, baa la njaa, ukosefu wa ajira sanjari na biashara haramu ya binadamu
mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki
kwa kushirikiana na AMECEA linapenda kujielekeza zaidi katika kuwasaidia maskini na
wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kama kielelezo cha imani tendaji.
CRS
linasubiri kusikia mikakati ya maendeleo ya AMECEA kwa kipindi cha miaka kumi ijayo,
ili liweze kuchangia kwa hali na mali katika utekelezaji wake, katika masuala ya kiufundi
na kifedha kama lilivyofanya kwa miaka mingine iliyopita. Ikiwa kama changamoto hizi
hazitashughulikiwa kikanilifu, kuna hatari kwamba, kiwango cha maendeleo kilichofikiwa
na Nchi za AMECEA kinaweza kuporomoka. CRS inapania kuendelea kuchangia utekeleza
wa miradi mbali mbali ya maendeleo inayoibiliwa na Majimbo Katoliki kutoka AMECEA.
Ushirikiano huu unajikita kwa namna ya pekee katika changamoto iliyotolewa
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuhusu mshikamano wa upendo, na kuridhiwa
na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kunako
mwaka 2012, mjini Kinshasa, DRC.