2014-07-21 11:38:24

Changamoto za kichungaji kutoka AMECEA


Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani limesema kwamba, litaendeleza ushirikiano na mshikamano na nchi za AMECEA ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Ushirikiano kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani na Kanisa Barani Afrika umekuwa ni wa manufaa kwa pande hizi mbili, tangu uhusiano huu ulipoanzishwa wakati wa utekelezaji wa Waraka wa kichungaji wa Papa Yohane Paulo II, Kanisa Barani Afrika, Ecclesia in Africa.

Hayo yamesemwa na Askofu Joseph W. Tobin, mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, mwishoni mwa juma, kwenye maadhimisho ya mkutano wa kumi na nane wa AMECEA unaoendelea mjini Lilongwe, Malawi. Anasema misaada ya kiutu na kimaendeleo imepokelewa kwa mikono miwili na Kanisa Barani Afrika na kwamba, kwa sasa wanataka kujielekeza zaidi katika kuwezesha majiundo makini ya mihimili ya Uinjilishaji mpya kwa Maaskofu Katoliki Kenya, Ethiopia na Tanzania.

Askofu Charles Kasonde wa Jimbo Katoliki la Solwezi, Zambia akiwasilisha mada yake kwenye mkutano wa AMECEA anabainisha kwamba, seminari na nyumba za malezi ni vituo muhimu sana kwa ajili ya kufunda mihimi ya Uinjilishaji Mpya Barani Afrika na kwamba, majiundo awali na endelevu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Mapadre. Kanisa linaendeleza dhamana na utume wake wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia na kwamba, hili ni jukumu la Wakristo wote, lakini Makleri wana mchango wa pekee!

Naye Askofu Paul Njiru Kariuki wa Jimbo Katoliki la Embu, Kenya katika mahubiri yake kwenye Ibada ya misa takatifu, iliyoadhimishwa hapo tarehe 19 Julai 2014 amewataka Mapadre kuiga mfano wa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa kwa kuonesha unyenyekevu na tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa.

Anasema, maadui wakuu wa Uinjilishaji mpya ni Makleri na waamini wanaoshindwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, changamoto kwa Taifa la Mungu katika nchi za AMECEA kuiga mfano wa Bikira Maria katika unyenyekevu na utayari wa kutekeleza mapenzi ya Mungu. Viongozi wa Kanisa wasaidie juhudi za kumpeleka Yesu Kristo katika familia na jamii inayowazunguka; kwa kuwafariji wale waliokata tamaa pamoja na kuwajengea uwezo maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii ili waweze kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha. Vijana wanapaswa kusaidiwa ili kuwa na mwelekeo makini wa maisha, vinginevyo watachanganyikiwa na kukosa dira ya maisha.

Askofu Kariuki anawakumbusha wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA kwamba, Bikira Maria alikuwa ni mwanamke aliyesheheni furaha, imani na matumaini, kama inavyojidhihirisha katika utenzi wa Bikira Maria, "Magnificati". Kumbe hata Kanisa katika nchi za AMECEA linapaswa kuwa ni kielelezo cha imani, matumaini na furaha.

Professa Clement Majawa kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA, anawahimiza Maaskofu wa AMECEA kuibua mbinu mkakati utakaopambana fika na vikwazo vya imani kwa watu wa nyakati hizi. Umefika wakati wa kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa Uinjilishaji Mpya ili kuwajengea waamini imani inayojielekeza katika ukweli, toba na wongofu wa ndani. Viongozi wa Kanisa hawana budi kuwaendea waamini wao huko waliko kwa kuanzia kwenye Familia ili kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji.

Kuibuka na kuenea kwa madhehebu ya Kikristo Barani Afrika, imani za kichawi na kishirikina, ibada za mashetani, ukabila, udini, uchu wa mali na madaraka na umaskini ni mambo ambayo yanaonesha udhaifu mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya kibinadamu: kiroho na kimwili. Imani kwa Kristo na Kanisa lake inapaswa kushuhudiwa katika matendo adili na manyofu. Mikakati ya Uinjilishaji mpya ipanie kuziba mianya ya utupu wa maisha ya kiroho inayowaandama waamini kwa kukazia toba, wongofu wa ndani na ushuhuda wa maisha.

Professa Clement Majawa anasema kwamba, Uinjilishaji Mpya ni mchakato unaokazia kwa namna ya pekee Katekesi ya kina kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili kadiri ya Amri za Mungu na Maisha ya Sala. Maisha ya kiroho hayana budi kuwa na uwiano na maisha ya kila siku, vinginevyo, Kanisa litakuwa na watu ndumilakuwili, wenye kubeba Biblia mikononi, lakini wanakesha usiku makaburini!









All the contents on this site are copyrighted ©.