2014-07-21 09:08:38

Bila unyenyekevu maisha ni patashika nguo kuchanika!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, katika kipindi kilichopita tulianza kutafakari juu ya familia kama shule ya fadhila. Kwa nafasi ya kwanza tukaitafakari fadhili ya unyenyekevu kwa sababu ya umuhimu wake. Tuendelee kuimarishwa na neno la Mungu lisemalo, “nyenyekeeni mbele ya Bwana, naye atawainueni” (Yak. 4:10). Bwana Mungu wetu hupendezwa na watu wanyenyekevu. Na kwa unyenyekevu wao huinuliwa, hujaliwa mema na hulindwa dhidi ya mabaya. RealAudioMP3

Tunapoitazama familia kama shule ya maadili, neno la mkazo kwa wazazi na wote wanaoshika dhamana ya malezi, ni kuhakikisha kuwa watoto wetu wanafundishwa unyenyekevu tangu mwanzoni. Tukitazama fujo tunazokuwa nazo ukubwani, tutaweza kugundua kuwa, hatukufunzwa kuwa wanyenyekevu udogoni.

Watoto wakilelewa na kukuzwa katika fadhila ya unyenyekevu, hao watajenga pia heshima kwa wote. Unyenyekevu kwa watoto unasaidia kujenga umoja wao na wataheshimiana. Watoto ndani ya familia wasipokuwa na unyenyekevu, hawatasaidiana, watadharauliana, watabaguana, watatengana katika makundi. Wapo watakaojiona ni watoto bora zaidi na wenye kustahili katika familia kuliko wengine. Na hapo ndipo unapoanza mgawanyiko usiotibika ndani ya Kanisa la nyumbani.

Watoto wakikomaa katika ubishi, kiburi, maringo na dharau, baadaye ukubwani wanakuwa ni wadau wa fujo na migomo isiyo na tija. Daima wataona wanakosewa haki hata pale wanapoelezwa mambo ya maana. Watoto wanyenyekevu ni tunu na amani ya familia na ni zawadi bora kwa Kanisa na Taifa.

Leo tusonge mbele kidogo, tuutazame unyenyekevu katika mashule na mahali popote pa kazi. Kwa hadhi yake, unyenyekevu hujenga amani na mazingira ya utulivu na usitawi katika jumuiya ya watu. Kama tulivyosema, unyenyekevu sio uzubavu, bali ni fadhila. Na ni fadhila ya watu wenye hofu ya Mungu tu. Kwa mtu asiyemcha Mungu, kwake unyenyekevu anaona kama ni upuuzi.

Unyenyekevu humweka kila mtu mahali pake, na humfanya aheshimu wengine. Endapo watu sio wanyenyekevu, hawatatambua vipaji vyao na wakavitumia vizuri, hawatatambua mapungufu yao ili wajirekebishe au kujijenga vizuri zaidi. Wachaji wa Mungu wanatuambia, unyenyekevu ni ngazi nzuri sana ya kujifahamu sisi wenyewe. Tukikosa unyenyekevu, tutajikataa na tutajikimbia wenyewe. Tutapenda kujionesha wema na wenye kufaa, kumbe sio.

Tunapeleka rai ya pekee mashuleni! Nako huko watu wafundishwe unyenyekevu. Fadhila ya unyenyekevu ipandikizwe kwa dhati kabisa ili kuunda watumishi wenye dhamiri safi yenye kuleta amani mahali pa kazi. Wanafunzi wanapopata tu elimu bila fadhila, hapo kuna hatari ya kuwa mashetani hodari. Watahitimu madarasa, na ikiwezekana watafaulu mitihani, pasipo kuelimika. Na aina hiyo ya wasomi ndiyo inayosumbua jamii leo. Unyenyekevu kwa mwanafunzi ni mlango wa usikivu na mafanikio. Popote pale, unyenyekevu ni lulu, ni faida.

Daima wanafunzi wasio na unyenyekevu, hupenda kujionesha kuwa wanajua na wanaweza, wakati hawawezi. Ndipo hapo tunapokuta utamaduni mkubwa wa wizi wa mitihani na kufaulishana kwa mbinu angamizi. Anayekwiba mtihani anataka aonekane amefaulu kumbe hakufaulu. Na ni kwa kukosa unyenyekevu, huyohuyo aliyefaulishwa kwa dharula, kesho na kesho kutwa anaingia katika uwanja wa kazi, tena kwa namna ileile ya mbinu. Bado hata hapo, kwa vile hakustahili na pia sio mnyenyekevu, ataharibu kazi na atawaharibia kazi wenzake. Na akiambiwa ameharibu kazi, kwa kukosa unyenyekevu, atasema anaonewa wivu.

Endapo wanafunzi wetu wanafundishwa unyenyekevu, watakuwa tayari kuyakubali yale ambayo hawayajui, ili waelekezwe vema. Watakubali maonyo na maelekezo, watakubali kusahihishwa wanapokosea na watakubali kusaidiwa pale wanaposhindwa. Lakini roho ya kujikweza kwa kiburi cha kuonekana tunajua kumbe hatujui, mwishowe tutaangamiza taifa na kanisa kwa huduma zetu zisizokidhi viwango.

Kutoka shuleni, tuhamie huko makazini kwetu! Unyenyekevu unahitajika pia mahali pa kazi. Wafanyakazi wanyenyekevu ni tunu na ni msaada mkubwa katika kujenga ufanisi. Wafanyakazi wasio wanyenyekevu ni mizigo na pia ni aibu kwa wenzao. Ni katika unyenyekevu mtu hujipokea katika maweza yake na mapungufu yake. Wafanyakazi wanyenyekevu hujenga amani mahali pa kazi. Ni katika unyenyekevu, mtu hupokea pia maweza ya wengine na mapungufu yao.

Hakika, kufanya kazi na watu wasio na unyenyekevu, ni kero kubwa. Daima watapenda kujionesha, kujisifusifu, kujitukuza, kutafuta makuu hata kwa njia ya kukanyaga pua za wenzao, watapenda umaarufu hata kwa njia ya kuwachafua wenzao, watadharau kazi za wenzao, hawataona chema katika wenzao, watadhulumu hata haki za wenzao. Katika mazingira kama hayo, ofisi huwa ni chungu na kazi haziendi.

Ofisi ya watu wasio wanyenyekevu hutawaliwa na matusi, wivu, kelele na ufanisi chini ya kisigino. Unyenyekevu wa kweli, ni mmoja ya siri za mafanikio kazini. Usichokijua vizuri, nyennyekea, omba wenzako wanaojua wakuelekeze. Ni katika unyenyekevu utajikuta unafundishwa mambo mengi mazuri yenye kukujenga zaidi. Neno linasema ‘majivuno ni mabaya’ (rej. Yak. 4:16)

Tutaendelea kipindi kijacho. Kutoka katika Studio za redio Vaticani ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.