Vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini na ukabila ni mambo yanayokwamisha
maendeleo ya wengi Barani Afrika!
Askofu Eduardo Hiiboro wa Jimbo Katoliki Tombura-Yambio, lililoko Sudan ya Kusini,
kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan lililopewa dhamana ya kupembua mada
inayohusu mazingira ya kitamaduni, kisiasa na kijaamii ambamo Kanisa linatekeleza
dhamana na utume wake, amewakumbusha wajumbe wa mkutano mkuu wa AMECEA unaoendelea
Jimboni Lilongwe, Malawi kwamba, kuna nchi kumi na saba Barani Afrika ambazo zinakabiliwa
na migogoro, kinzani na vita.
Kutokana na hali kama hii, Kanisa halina budi
kuwa ni sehemu ya mchakato wa majadiliano yanayolenga kutafuta suluhu ya amani ya
kudumu Barani Afrika. Kanisa lisaidie kuhakikisha kwamba, sera za kijamii, kisiasa
na kiuchumi zinalenga kudumisha na kukuza utu na heshima ya binadamu.
Ukosefu
wa misingi na kanuni za utawala bora ni kati ya mambo yanayochangia kugumisha mchakato
wa Uinjilishaji Mpya katika baadhi ya nchi za AMECEA. Afrika ya Mashariki kwa sasa
inakabiliwa na vitisho vya vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini pamoja na
udani; mambo ambayo yanahatarisha haki, amani na utulivu Sudan, Sudan ya Kusini, Kenya,
Somalia na Tanzania. Mashambulizi na mauaji ya kigaidi yanayoendelea kusikika sehemu
mbali mbali za Afrika Mashariki na kati yanatishi amani na mustakabali wa maendeleo
ya watu: kiroho na kimwili.
Kuna haja kwa viongozi Barani Afrika kuhakikisha
kwamba, wanajikita kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi; kusimamia vyema rasilimali
ya taifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote kwa kuondokana na tabia
ya ubinafsi inayojengeka miongoni mwa wananchi wa Bara la Afrika kwa kupenda mno fedha
na mali, kiasi cha kutumbukia kwa urahisi katika saratani ya rushwa, ufisadi na wizi
wa mali ya umma. Uchu wa madaraka ni tatizo na changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi
kwa umakini mkubwa, vinginevyo, Bara la Afrika litaendelea kuwa ni uwanja wa fujo.
Kanisa
Katoliki Barani Afrika limekuwa likichapisha nyaraka za kichungaji, kwa kutumia Tume
ya haki na amani, Ibada na huduma katika taasisi ya elimu ya juu. Mbinu hizi zote
bado hazijazaa matunda yanayokusudiwa. Kuna haja kwa Maaskofu wa AMECEA kuibua mbinu
mkakati utakaowashirikisha wanataaaluma Wakristo katika kufikisha hoja na utekelezaji
wake. Kanisa liendelee kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu
na kuzuia kinzani na mipasuko ya kijamii pale inapowezekana!