Muda wa longo longo umekwisha, watu wanataka kuona maendeleo!
Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Afrika na Madagascar, SECAM, amewataka Waafrika kutoa maana ya kweli kuhusu maendeleo
endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Hii ni changamoto
iliyotolewa na SECAM wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Siku mbili lililofanyika
kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbainiana, kilichoko mjini Roma kwa ajili ya kuwaenzi
watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II, ambao wamechagia kwa kiasi kikubwa katika
ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika.
Kongamano hili liliongozwa na
kauli mbiu Kanisa Barani Afrika: kutoka Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hadi mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo: mchango wa Papa Yohane XXIII na Yohane Paulo II.
SECAM
inasema, kuna haja kwa wananchi wa Bara la Afrika kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali
watu, fedha na vitu katika mchakato wa kujiletea maendeleo yao wenyewe kuliko tabia
ya sasa ya kutegemea misaada kutoka ng’ambo hali ambayo inadhalilisha utu na heshima
ya wananchi wa Bara la Afrika. Hii inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya misaada inayotolewa
imekuwa na masharti makubwa ambayo wakati mwingine yanakwenda kinyume cha utu na maadili
mema.
Familia ya Mungu Barani Afrika ilitumia fursa ya kuwatangaza watakatifu
Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuangalia jinsi ambavyo Kanisa barani Afrika limeendelea
kumwilisha Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na
utume wake. Kanisa Barani Afrika linaendelea kujipanga vyema zaidi ili kuchangia katika
ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika, kwa kutoa taswira na utambulisho ulio sahihi
zaidi, kwa njia ya majadiliano katika jukwaa la imani, tamaduni na maendeleo endelevu.
Kongamano
hili la Kimataifa limehudhuriwa na Makardinali, Maaskofu, Mabalozi, wanataalimungu
na falsafa kutoka Barani Afrika, Wanafunzi kutoka vyuo vikuu vilivyoko mjini Roma
na viunga vyake. Kwa hakika ni Kongamano ambalo lilikuwa limesheheni matumaini ya
Familia ya Mungu Barani Afrika.
Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la
Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum, katika hotuba yake ya ufunguzi
alisikitika kusema kwamba, Familia ya Mungu Barani Afrika inakumbana na na changamoto
mbali mbali zinazoibuliwa kutoka katika utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Lakini Bara la Afrika linapaswa kukumbuka kwamba, lina mchango mkubwa katika ustawi
na maendeleo ya Kanisa la Kiulimwengu, dhana inayopaswa kufanyiwa kazi kwa ari na
bidii kubwa zaidi. Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni
amepongeza uhusiano unaoendelea kujengeka kati ya Baraza lake na SECAM katika kukuza
na kudumisha majukwaa ya utamaduni na kwamba, Baraza lake, linataka kuwekeza zaidi
katika ustawi wa Kanisa Barani Afrika.
Kwa ufupi mada zilizochambuliwa katika
kongamano la siku mbili kama sehemu ya mchakato wa kuwaenzi Watakatifu Yohane XXIII
na Yohane Paulo II zimegusia kuhusu: Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na utekelezaji
wake kwa Kanisa Barani Afrika; mchango wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican
na Mapapa waliofuatia na utekelezaji wake na Kanisa Barani Afrika.
Wataalam
pia waligusia mwangwi wa kazi zilizofanywa na Chama cha wanataalimungu Barani Afrika,
(ATA) kuhusu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Mchango wa Papa Yohane XXIII na Yohane
Paulo II Barani Afrika pamoja na mageuzi yaliyojitokeza Barani Afrika mara tu baada
ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Imeandaliwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.