2014-07-19 09:35:10

Mshikamano wa dhati kati ya Kanisa na Familia Barani Afrika!


Bara la Afrika halina budi kujikita katika mchakato utakaoliwezesha kujenga na kuimarisha mshikamano kati ya wazee, vijana na watoto unaosimikwa katika umoja na upendo kati ya Kanisa na Familia, ili kukabiliana kwa dhati na changamoto zinazotolewa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknlojia dhidi ya taasisi ya familia.

Ni changamoto inayotolewa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia kwa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA unaoendelea mjini Lilongwe, nchini Malawi. Maaskofu zaidi ya 250 kutoka katika nchi za AMECEA wanashiriki na kauli mbiu inayoongoza ni "Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo".

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa katika awamu kuu mbili. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Mababa wa Sinodi wanatoa mapendekezo yatakayoliwezesha Kanisa kukabiliana na matatizo na changamoto dhidi ya familia, ili kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa. Hii ni changamoto si tu kwa Mama Kanisa bali hata kwa Serikali na vyama vya kiraia. Familia kwa sasa iko njia panda, kwani kuna mambo ambayo yanachangia kuhatarisha upendo, umoja na mshikamano wa dhati ndani ya familia.

Familia Barani Afrika zinakabiliwa na changamoto kubwa, ili kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu mapokeo, mila na desturi njema za Kiafrika. Familia ni shule ambamo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili zinarithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kwa kizazi kingine, changamoto ya kuendelea kuenzi Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaolisakama Bara la Afrika kwa kasi ya ajabu. Mitara, utoaji mimba, ukabila na udini ni mambo ambayo yanahatarisha misingi bora ya maisha ya ndoa na familia.

Askofu mkuu Paglia anasema hatari kubwa inayozinyemelea Familia nyingi kwa sasa ni pamoja na: ubinafsi, uchoyo, uhuru pasi na mipaka unaohatarisha tunu msingi za maisha adili na matakatifu na kusahau kwamba, familia ni nguzo msingi ya maisha ya kijamii, inayopaswa kulindwa, kutetewa na kuendelezwa. Wanandoa hawana budi kuwa mwili na roho moja, ili kushinda kishawishi cha ubinafsi kinachoweza kubomoa misingi ya ndoa, utu na maadili mema.

Wanandoa na familia wanakumbushwa kuzingatia misingi ya maisha ya ndoa kama inavyobainishwa na kufafanuliwa katika Maandiko Matakatifu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ambalo kimsingi ni Familia ya Mungu, zinahamasishwa kuyatakatifuza malimwengu katika medani mbali mbali za maisha, kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili.

Hapa wanafamilia hawana budi kuwa mstari wa mbele katika kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kwa kuonesha pia uzuri wa maisha ya ndoa na familia. Familia zijitahidi kujikita katika fadhila ya uaminifu na udumifu, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati kati ya Familia na Kanisa.

Haki za watoto ndani ya familia hazina budi kulindwa na kuheshimiwa, ili watoto hao waweze kuzaliwa, kulelewa na kuonja upendo wa wazazi wao wawili, yaani Baba na Mama kadiri ya mapenzi ya Mungu. Watoto waonjeshwe Injili ya Uhai kwa kulindwa na kupewa tiba wanazostahili, hakuna sababu ya mtoto yoyote kuuwawa kwa sababu ya imani za kishirikina au kwa sababu ya ulemavu fulani.

Sera na mikakati ya kiuchumi ipanie kuzisaidia familia kutekeleza wajibu wake msingi na kamwe zisidhulumiwe wala kudhalilishwa; changamoto kwa wanasiasa, wachumi na watunga sera. Hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo, nguvu na ari mpya itakayosaidia kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa, familia na maisha, dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kanisa likifanikiwa kutekeleza dhamana na malengo yake katika kulinda, kutetea na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, itakuwa ni rahisi kuwashirikisha waamini wa dini na madhehebu mengi ili kulinda na kuendeleza familia ambayo kimsingi ni urithi wa binadamu na ianayopaswa kuishi katika msingi wa amani na mapendo!







All the contents on this site are copyrighted ©.