2014-07-19 11:49:58

Kanisa liko juu katika huduma kwa wananchi wa Kenya!


Mama Margaret Uhuru Kenyatta, Mke wa Rais Kenyatta wa Kenya amelishukuru na kulipongeza Kanisa Katoliki nchini Kenya kwa kujipambanua kikamilifu kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu kwa wananchi wa Kenya. Ni jukumu la waamini walei kushikamana na Kanisa pamoja na taasisi zake katika kuchangia mikakati ya maendeleo ya watu.

Mama Margaret Kenyatta ameyasema hayo, mwishoni mwa Juma wakati wa kuchangia harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya Parokia ya Mwenyeheri Josefu Allamano, Jimbo kuu la Nairobi. Ameipongeza Parokia kwa huduma ya afya, utunzaji bora wa mazingira na utume kwa vijana. Mikakati hii ya maendeleo inachangia kwa kiasi kikubwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Kenya katika kuwaletea wananchi wake maboresho ya maisha katika sekta ya afya, elimu na utunzaji bora wa mazingira pamoja na kuwawezesha vijana kielimu na kimaadili.

Kanisa Katoliki nchini Kenya ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu kwani linamiliki na kuendesha shule za awali zipatazo 4, 169 zinazotoa elimu kwa watoto 335, 285: Kanisa pia linamiliki na kuendesha shule za msingi 4, 769 zinazowahudumia wanafunzi 2, 393, 658. Shule za Sekondari ni 1618 ambazo zina wanafunzi 737, 508 pamoja na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA.

Kanisa Katoliki nchini Kenya linamiliki na kuendesha hospitali 184, Zahanati 390, Vituo vya wagonjwa wa ukoma 22; nyumba za wazee na wagonjwa ni 86. Kuna vituo vya watoto yatima 401 vinavyowahudumia watoto 1, 334 kadiri ya takwimu za Kanisa Katoliki kwa mwaka 2012.







All the contents on this site are copyrighted ©.