2014-07-19 12:16:05

AMECEA isaidie kukoleza imani!


Askofu mkuu Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia, katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kazi kubwa ya kimissionari iliyofanywa na Wamissionari pamoja na kuombea amani katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA, Ijumaa tarehe 18 Julai 2014, amelitaka Kanisa kuwa kweli ni chombo cha imani kwa ajili ya Familia ya Mungu katika nchi za AMECEA. Kanisa bado linakumbu kumbu hai ya sherehe za kutangazwa kwa Papa Yohane wa XXIII na Papa Yohane Paulo II kuwa watakatifu.

Askofu mkuu Souraphiel amewataka Maaskofu wa AMECEA kujifunza kutoka kwa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliyeamua kwa utashi wake kamili kung'atuka kutoka madarakani na hivyo kutoa nafasi kwa Papa Francisko ambaye ameonesha unyenyekevu kwa kuomba sala kutoka kwa waamini pamoja na kuendelea kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu.

Watu wanaendelea kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Waamini wanapaswa kuwa na matumaini katika nguvu ya sala na kamwe wasikate tamaa. Papa mstaafu Benedikto XVI anaendelea kulitegemeza Kanisa kwa njia ya sala zake. AMECEA wakati huu inaweza kutafakari kuhusu mchango wa Kanisa katika kuwaendeleza wananchi wa AMECEA.

Wakati huo huo, Padre Benedict Ssettuuma, wakati akiwasilisha mada yake anasema, Wamissionari wa kwanza Barani Afrika walijitahidi kusoma alama za nyakati ili kutekeleza mikakati ya Uinjilishaji wa awali, kiasi kwamba, leo hii Ukristo umeota mizizi katika Nchi za AMECEA.

Wamissionari walisafiri sana, wakasali na kueneza Ibada mbali mbali ambazo zimejikita katika mioyo ya waamini hadi leo. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuendeleza mchakato wa utamadunisho, ili Kanisa liweze kuota mizizi katika maisha na vipaumbele vya waamini sanjari na kuendeleza kazi na utume ulioanzishwa na Wamissionari.

Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kupambana na kufa na kupona na umaskini, ujinga na maradhi mambo ambayo yanawaandama watu pamoja na kuendelea kuwatangazia Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Bado kuna haja ya kukuza na kudumisha Ibada mbali mbali zinazojikita pia katika ushuhuda wa maisha, ili kuleta mvuto na mashiko kwa majirani!







All the contents on this site are copyrighted ©.