2014-07-18 11:51:22

Takukuru na umma ni sawa maji na samaki!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini kuhakikisha kuwa kesi za rushwa dhidi ya watu mbali mbali inazozipeleka mahakama zinakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa maana ya washitakiwa kukutwa na makosa. Aidha, Rais Kikwete ameitaka Taasisi hiyo kuwa karibu na umma akisema kuwa TAKUKURU na umma ni sawa na maji na samaki kwa sababu Taasisi hiyo haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na umma.

Rais pia amesema kuwa Serikali yake inakusudia kutunga sheria ya kuwalinda watoa habari kwa TAKUKURU ili kufanikisha zaidi kazi ya Taasisi hiyo. Rais Kikwete ameyasema hayo Alhamisi, Julai 17, 2014, kwenye siku yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku sita mkoani Ruvuma ambako ameanzia ziara yake kwa kutembelea Songea Mjini.

Katika siku yake ya kwanza, Rais Kikwete ambaye anafuatana na Mama Salma Kikwete, amezindua ghala kubwa la kuhifadhia chakula lililojengwa na Wakala wa Taifa wa Kuhifadhji Chakula (NFRA), amezindua nyumba za bei nafuu ambazo zimejengwa katika eneo la Mkuzo na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), amefungua rasmi Ofisi za TAKUKURU za Mkoa wa Ruvuma na pia amehutubia mkutano mkubwa wa hadhara kwenye Uwanja wa Majimaji wa Songea.

Akizindua ofisi hiyo ya TAKUKURU, Rais Kikwete ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikiboreka kila mwaka lakini akasisitiza kuwa wakati umefika kwa TAKUKURU kufiksha mahakamani kesi zile ambazo zina nafasi kubwa ya kutuhumiwa kukutwa na hatia. "ni vyema tuhakikishe kuwa kesi zinazokwenda mahakamani zinakuwa na mpangilio mzuri na nafasi kubwa ya Serikali kushinda kesi hizo."

Ameongeza Rais Kikwete: "Ni vyema pia kuwa pamoja na mafanikio yote ya TAKUKURU ni lazima taasisi hiyo iongeze ushirikiano wake na umma. TAKUKURU na umma ni sawa na samaki na maji kwa sababu kama ilivyo kuwa samaki hawezi kuishi nje ya maji, hivyo hivyo TAKUKURU haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano na umma, bila kupata habari kutoka umma."

Ofisi hiyo ya TAKUKURU ya Mkoa wa Songea imegharimu sh. bilioni 1.18 na imejengwa kwa kiasi cha miezi 20 ikiwa ni sehemu ya sera ya Serikali ya kujenga ofisi tatu za mikoa kila mwaka ili kuondoa uhaba wa ofisi za kufanyika kazi za Taasisi hiyo. Kwenye uzinduzi za nyumba za NHC, Rais Kikwete ameambiwa kuwa katika eneo hilo la Mkuzo, shirika hilo limejenga kiasi cha nyumba 18 za kuuza na zimejengwa kwa gharama ya sh. milioni 676.

Rais Kikwete pia ameambiwa kuwa nyumba hizo zimejengwa katika kutekeleza kaulimbiu ya NHC ya "Nyumba yangu, Maisha yangu" ambayo mpaka sasa inatekelezwa katika mikoa 14. Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Januari mwaka jana na unakamilika mwezi ujao, Agosti, 2014. Nyumba hizo, ameambiwa Rais Kikwete, kuwa zitauzwa kwa gharama ya kati ya sh. milioni 33 na 44 bila kodi ya VAT lakini ambayo inaongezeka na kuwa kati ya milioni 44 na 52 kwa kutegemea ukubwa wa nyumba - kuanzia ya vyumba viwili hadi nyumba vitatu. Rais Kikwete anaendelea na ziara yake mkoani humo.








All the contents on this site are copyrighted ©.