2014-07-18 10:13:53

Mitandao ya kijamii ni fursa za Uinjilishaji!


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil limeandaa semina ya siku tatu kwa ajili ya vijana wanahabari, semina itakayoanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 27 Julai 2014, huko Aparecida, kwa kuongozwa na kauli mbiu "Mitandao ya kijamii ni fursa ya mawasiliano kwa ajili ya Uinjilishaji nyakati za utamaduni wa digitali. Hii ni semina ya nne kuwahi kuandaliwa na Idara ya habari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil na mara ya pili semina hii kufanyika katika ngazi ya kitaifa kwa ajili ya vijana nchini Brazil.

Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anatarajiwa kushiriki katika semina hii kwa njia ya video. Atazungumzia kuhusu uhusiano uliopo katika mchakato wa mabadiliko ya kijamii na kitamaduni mintarafu maendeleo ya teknolojia ya digitali.

Padre Antonio Spadaro, Mkurugenzi mkuu wa Jarida la Wayesuit "Civiltà Cattolica" anatarajiwa kupembua kwa kina na mapana uhusiano kati ya Uinjilishaji na tasaufi katika mitandao ya kijamii. Washiriki wa semina hii watawezeshwa pia kujikita katika uelewa wa taalimungu katika mitandao ya kijamii sanjari na uwepo wa mitandao ya kijamii inayosimamiwa na kuratibiwa na Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini. Wajumbe wanapewa mbinu za sanaa ya kuzungumza na kuinjilisha; wasemaji wakuu wa Kanisa pamoja na dhana ya Umissionari kwenye mitandao ya kijamii.









All the contents on this site are copyrighted ©.