2014-07-18 12:25:03

AMECEA wasikitishwa na ukosefu wa uhuru wa kidini kwa baadhi ya nchi!


Askofu mkuu Tarcisio Ziyaye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA katika hotuba yake ya kuwakaribisha wajumbe wa AMECEA, Alhamisi, tarehe 17 Julai 2014 amewashukuru viongozi wa nchi za AMECEA kwa kukuza na kuendeleza uhuru wa kuabudu miongoni mwa wananchi wao, kielelezo kwamba, wote ni Familia ya Mungu, licha ya tofauti zao za kidini, kijamii, kisiasa na kitamaduni.

Wajumbe wa AMECEA huku wakiongozwa na kauli mbiu ya maadhimisho ya kumi na nane ya mkutano wake mkuu, wanapenda kujielekeza zaidi katika kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu, ili waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kukumbatia na kimwilisha tunu msingi za Kiinjili, zilizohubiriwa na Yesu Kristo mwenyewe. Waamini kwa upande wao, wanahamasishwa kuwa kweli ni mashahidi wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika medani mbali mbali za maisha, ili kuyatakatifuza malimwengu.

Askofu mkuu Ziyaye anasema, mkutano mkuu wa AMECEA utaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika masuala ya Uinjilishaji, toba na wongofu wa ndani pamoja na uhsuhuda wa imani. AMECEA inaishukuru Serikali ya Malawi kwa mapokezi na ukarimu ambao wamewaonjesha wajumbe wa mkutano mkuu wa AMECEA pamoja na kuzishukuru Serikali husika kwa kuhakikisha kwamba, zinaendeleza na kudumisha uhuru wa kuabudu na hivyo kuwawezesha Maaskofu wa AMECEA kutekeleza wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ufanisi na tija.

Maaskofu wa AMECEA wanasikitika kwa nchi zile ambazo uhuru wa kidini haukuheshimiwa wala kuthaminiwa; wanaonesha mshikamano wao wa dhati na Wananchi wa Sudan ya Kusini ambao kwa sasa wanakabiliana na hali tete ya kisiasa kutokana na machafuko ya vita yanayoendelea nchini humo. AMECEA inaombea haki, amani utulivu na upatanisho wa kitaifa sanjari na kuendeleza mshikamano wa kimataifa na Kanisa la Kiulimwengu.







All the contents on this site are copyrighted ©.