Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 16 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Mpendwa mwana wa Mungu, tunatafakari Neno la Mungu Dominika ya 16 ya mwaka A wa Kanisa.
Wewe nami tunaalikwa tena kutambua kuwa huruma ya Mungu ni ya milele na ni kwa ajili
ya wadhambi na waliowema.
Kamwe Mungu
hataweza kumpatiliza awaye yote aombaye huruma yake na kutubu. Tunaambiwa hata kama
dhambi za mtu huyu zingekuwa nyekundu kiasi gani, Mwenyezi Mungu atazigeuza na kuwa
nyeupe. Hata hivyo yatupasa kutambua pia kuwa Mungu ni mwenye haki, kumbe kama mmoja
hataacha njia yake mbaya, mwishoni atakuwa ni chukizo na hivi kutupwa nje ya ufalme
wa Mungu.
Mpendwa mwana tafakari, katika somo la kwanza tunaona jinsi mwandishi
anavyojaribu kuwaimarisha wana wa Israeli ili kuwatoa katika wasiwasi walionao. Waisraeli
wanajiuliza mbona mambo yetu na hasa katika uwanja wa biashara hayafanikiwi? Mbona
wapagani wasiomcha Mungu wanafaulu katika shughuli zao? Wana wa Israeli wangependa
Mungu awapatilize wapagani wasiomcha Mungu! Ndiyo kusema wale wote wafanyao ubaya
hivi leo, wangepaswa kupatilizwa na kupotea kabisa toka uso wa nchi!
Basi tokana
na mtizamo huo mwandishi wa somo la kwanza anawajibu na anatujibu sisi hivi leo kuwa
Mungu ni upendo mkamilifu ambao haubagui awaye yote badala yake ni kwa ajili ya wema
na wabaya. Mungu wetu hawafanyi watu waamini kwa njia ya mabavu bali hujiingiza katika
historia ya maisha yao na kuwageuza taratibu, ndiyo kusema Roho wa Mungu, aliye Roho
wa upole, mfariji, Roho wa elimu na hekima ya kimungu, hutoa nafasi kwa wadhambi watubu
na kisha wamwendee yeye katika uhuru kamili wa wana wa Mungu.
Ujumbe huu unajionesha
wazi katika injili ambapo tunaona Mwana wa Mungu anasiha mbegu ya imani na mbele yake
kuna wapinzani walioadui wa mbegu hiyo. Je mwana wa Mungu atawapatiliza hawa maadui
wa imani? Hapana, daima ana subira kwa ajili yao, akiwajalia Roho wa elimu na hekima
ili polepole watubu na kuiacha njia yao mbaya. Hata hivyo kama hawatapokea zawadi
hiyo ya toba basi haki ya Mungu hutenda kazi yake.
Mtakatifu Paulo anasisitiza
daima kuwa tunapaswa kuomba paji la Roho Mtakatifu ili kuweza kutusaidia kuhuisha
sala yetu iliyodhaifu ili ipate uhakika wa kupokelewa na Mungu Baba. Kwa paji la Roho
Mtakatifu mwanadamu anageuka kuwa dhabihu safi mbele ya Mungu. Kwa paji la Roho Mtakatifu
mwanadamu anaweza kugundua huruma ya Mungu iliyo kuu ambayo huja kama mvua kwa ajili
ya wote. Mwanadamu pia ataweza kuona katika Neno la Mungu kuwa Kristo Mkombozi alikuja
si kwa ajili ya wema tu bali kwa ajili ya wote.
Mpendwa mwana wa Mungu, Neno
la Mungu daima hutualika kukubali tukiwa na utulivu wa moyo uwepo wa dhambi katika
ulimwengu. Kukubali uwepo wa dhambi si kukumbatia dhambi bali utambuzi unaosaidia
kuanza vita vya kiroho dhidi ya dhambi hiyo. Tunapigana vita tukiwa na uhakika kwamba
Kristu ameishinda dhambi na siku moja upendo wa Mungu utafuta yote. Hili latudai unyenyekevu,
maisha ya sala na utafiti wa kiinjili tukiulekea msalaba wa Kristu. Tumsifu Yesu Kristu.
Tafakari hii imeletwa kwenu na Padre Richard Tiganya C.PP.S.