2014-07-17 10:35:15

Shuhudieni ukweli!


Askofu mkuu Socrates Villegas, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini anasema, Jamii ambayo haijajisimika katika msingi wa ukweli, itayumba na kamwe haitakuwa na uwezo wa kusonga mbele na kwamba, itashindwa kujenga mahusiano bora na thabiti ya maisha ya kijamii na matokeo yake, watu watashindwa kuwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi! RealAudioMP3

Huu ni ujumbe ambao Askofu mkuu Villegas amewatumia wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano kongamano la Uinjilishaji mpya lililofanyika hivi karibuni mjini Pasay, kwa kuwashirikisha watu zaidi ya elfu nne kutoka Majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Ufilippini. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutafuta kilicho chema, kilicho kweli na cha haki, kwa kuzingatia kanuni ya upendo kwa Mungu na jirani; mambo yanayojikita katika mshikamano na huduma kwa jirani, lakini zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Askofu mkuu Villegas anasema, Uinjilishaji Mpya ni mchakato wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu unaojikita katika ushuhuda wa kweli za Kiinjili zinazotolewa na Yesu Kristo kwa ajili ya binadamu, ili ziweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya binadamu. Hapa kuna haja ya watu katika tamaduni na historia yao kuwa wazi kwa Yesu anayeendelea kutembea bega kwa bega na Kanisa lake. Kumbe, kiini msingi cha Uinjilishaji Mpya ni Ukweli.

Hapa waamini wanahamasishwa kutafuta, kuzungumza na kumwilisha ukweli katika uhalisia wa maisha yao. Kwa namna ya pekee, waamini walei wanaalikwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ukweli wa maisha, kwa kuchangia katika mchakato wa mikakati ya maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa njia hii watakuwa wanashiriki kikamilifu katika Uinjilishaji Mpya, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.

Uinjilishaji ujikite katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo wenye mvuto na mashiko hasa kwa wale ambao wamesahau mlango wa Kanisa kutokana na sababu mbali mbali za maisha! Hawa wale ni walengwa wa kwanza wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Waamini wanaalikwa kuonesha kwa namna ya pekee, uwepo endelevu wa Kristo katika maisha na utume wa Kanisa, katika Sakramenti na Neno la Mungu.

Naye Kardinali Gaudencio Morales, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Manila, anawataka waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Ufilippini kuendeleza na kudumisha huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kwa njia ya matendo ya huruma. Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anawatumia kama vyombo vya huduma makini kwa jirani na maskini.

Watu wamekirimiwa mengi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hakuna mtu anayeweza kulalama kwamba, hana hata kitu kidogo cha kutoa kwa ajili ya kuwahudumia maskini, hata maskini wanalo jambo ambalo wanaweza kushirikisha kwa ajili ya kuwahudumia maskini wenzao. Ushuhuda wa upendo ulenge kuboresha huduma inayotolewa na Kanisa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya watu.

Waamini walei kwa namna ya pekee kabisa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni vyombo vya ukweli, huruma na upatanisho kati ya watu ndani ya Jamii kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, mwanadamu akiheshimuwa na Mwenyezi Mungu akitukuzwa na kuabudiwa kwani Yeye ndiye asili ya maisha na utu wa binadamu.








All the contents on this site are copyrighted ©.