2014-07-17 16:01:28

Anawachimbia mkwara mzito!


Leo tunaendelea bado kuona mifano juu ya ufalme wa mbingu inayomhusu mkulima. Yesu anawasimulia mfano wa pili wale walio nchi kavu: “Akawatolea mfano mwingine” Mfano unasema: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake.”

Mpandaji au muumbaji ni Mungu mwenyewe aliye mwema na vyote alivyoviumba ni vyema kama inavyosemwa mara saba katika kitabu cha Mwanzo juu ya uumbaji: “Mungu akaona ya kuwa ni vyema.” Hata hivyo tunajiuliza: Kama Mungu aliona kila kitu alichoumba kuwa ni chema, kulikoni tunaona uovu na ubaya. Uovu huu imeibukaibukaje na umesababishwa na nani kama siyo na Mungu mwenyewe? Ndivyo watumwa wanavyomwuliza mwenye nyumba: “Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako?”

Mwenye nyumba anajibu: “Watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.” Kwa hiyo adui aliyepanda mbegu ya uovu ni shetani. Hata hivyo bado tunaweza kumwuliza Mungu, kwa nini basi asimzuie au asimwadhibu huyo shetani anayeharibu kazi yake njema?

Baada ya kuona mazingira haya sasa unaalikwa kuangalia tofauti kati ya swali la watumwa na jibu la mwenye shamba. Watumwa wanamwomba mwenye nyumba ruhusa ya kuingilia kati: “Je, wataka twende tukayakusanye magugu?” Mwenye nyumba akawajibu: “La, msije mkakusanya na kuzing’oa ngano pamoja nayo.” Ni dhahiri kwamba mmea wa ngano na wa magugu unapokuwa bado mchanga hufanana sana hivi ni rahisi kuzichanganya mpaka zinakapokua na kutoa matunda ndipo unaweza kuona tofauti kati ya ngano na magugu.

Katika mfano huu, Yesu anataka kutuambia kwamba, magugu hayo ni sisi wenyewe yaani “adui wa mtu ni mtu mwenyewe.” Wema na ubaya katika mtu ni rahisi sana kuchanganya hadi yanapotokea matunda. “Kwa matunda yao mtawatambua”. Magugu au uovu upo ndani ya mtu mwenyewe, na kama hachukui tahadhari, uovu huo utamharibu mtu, utamtoa maisha, utamfanya asiwe binadamu mwenye utu.

Magugu hayo ndani mwako yana majina yanayoeleweka, nayo ni: uchu, tamaa, uroho, kujiona, shauku hasa ya kujikusanyia mali. Tamaa ya kutaka kutawala na kukandamiza wengine ya kupenda kujionesha na kuufurahia ubinafsi wa kujifikiria wewe wenyewe. Magugu au uovu huo tunazaliwa nao na unaitwa “dhambi ya asili.” Daima tunafikiria kuwa Mungu angetakiwa kuumba ulimwengu usio na mapungufu yoyote.

Kumbe, mapungufu hayo Mungu hawezi kuyafuta kwa sababu kwa kufanya hivyo itambidi aharibu kabisa ulimwengu huu na kuuumba ulimwengu mwingine yaani, kama anauharibu uovu ulimwenguni, itamaanisha kutuharibu sisi pia. Kwani hiyo ndiyo hali yetu halisi.

Magugu yaliyotapakaa ulimwenguni kama vile vita, kukoseana haki, kuchukiana, kuoneana, kubaguana kijinsia, wivu, udanganyifu, rushwa, ubakaji, nk, hayo yote ni sehemu ya sisi wenyewe na yanapandwa na tabia yetu wenyewe. Yesu anataka tuione hali hii halisi ya maisha na tujihadhari, vinginevyo uovu huo utatusababishia hasara kubwa zaidi.

Yabidi kuelewa kwamba, hali halisi ya maisha ya binadamu hapa duniani ni ya ukinzani, ni ya mgongano na upinzani wa kudumu, kama vile ukinzani ulioko kati ya giza na mwanga, na kati ya wema na ubaya. Yabidi kuikubali mipaka hiyo kwa vile ni hali halisi ya maisha. Pale ambapo hali hizo hazikupokewa kama sehemu ya hali yetu ya kibinadamu mapato yake mtu unaweza kukosa uvumilivu dhidi yako mwenyewe na ya wengine.

Usipojipokea na kujikiri utajikuta ni katili na kuwaka hasira, unajikasirikia mwenyewe, unawakasirikia wenzako na unamkasirikia hata Mungu kwa sababu unashindwa kujipokea mwenyewe kitulivu. Kumbe yatakiwa pale unapokosea, ujikubali na kusema “Nimekosea na sasa yabidi nianze upya kitulivu safari yangu kuelekea kwenye maisha.”

Wakati wa mavuno Bwana wa nyumba atawaambia watumwa wale: “Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.” Moto pekee unaojulikana kwa upande wa Mungu ni moto wa Upendo wa Mungu mwenyewe, moto wa Neno lake, moto wa Roho yake. Moto huo ndiyo unaoweza kufifisha magugu na kuiacha ngano nzuri istawi.

Wanafunzi wanamwomba Yesu: “Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.” si kweli kwamba hawakuelewa mfano huu, bali hawakutaka kupokea. Hao mitume ni sawa tu na sisi leo ambao baada ya kusikiliza ujumbe wa Bwana, tunabaki bado tumeikasirikia hali yetu ya kibinadamu ambayo siyo kamili.

Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba mitume hao wanaona upande mbaya tu wa mambo, yaani katika shamba la Bwana wao wanayaona magugu tu na kuisahau ngano. Ndivyo tufanyavyo binadamu, katika mazingira maovu sisi tunaona uovu tu, tunasahau kuona upande mzuri, yaani upande mwema wa ubinadamu.

Ujumbe wa mwisho anaotupatia Bwana ni hatima ya magugu na ngao. Ni hatima tunayopenda kuisikia kwamba: “Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao.”

Sehemu hii inapendeza kuisikia kwamba waovu watatupwa motoni na wema wataingia paradisini. Kila mmoja apate haki yake. Namna hii ya kuelewa mfano huu ni finyu kabisa na inapingana na ukweli mzima wa mfano huu wa Yesu, kwa sababu endapo mambo yatakuwa hivyo, basi huko motoni kwenye makao ya ibilisi hayatatupwa magugu peke yake yaani watu wabaya tu, bali zitatupwa hata ngano njema, kwa sababu ndani ya kila mtu kuna wema na ubaya.

Hivi atatupwa mtu mzimamzima mwenye wema na ubaya. Kumbe lugha hii ya ufunuo iliyotumika hapa inataka kutuonesha umuhimu wa maisha tunayoyaishi hapa ulimwengu. Kwamba maisha haya yatakuwa na matokeo ya milele. Endapo sisi hatufanyi chochote cha kukuza mbegu njema iliyo ndani yetu ili ikue na kuzaa matunda mazuri ndani yetu, na badala yake tunauenzi uovu wa hali yetu ya kibinadamu basi sehemu kubwa ya maisha yetu itakuwa imepotea bure.

Hapo kweli tutajijutia wenyewe tutakapojiona kuwa tumepoteza muda bure hapa duniani kwa kutenda uovu usio na nafasi ya kudumu, na huko ndiko kunastahili kulia na kusaga meno. Lakini wakati huo kilio hicho hakitasaidia chochote, kwa vile itakuwa kama “majuto ni mjukuu.”

Kwa hiyo, Habari njema hapa ni kwamba mwishoni magugu yote yatakusanywa na kuchomwa na itabaki ngano tupu, yaani tunda zuri lililo ndani ya kila mtu ndilo litakalobaki. “Wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao.” Hii ndiyo hatima na tamati ya historia ya ulimwengu huu mzuri alioumba Mungu hata kama mipaka au kasoro hii imesababisha magugu mengi. Wema na Upendo ndivyo vitakavyopeta mbele ya Mungu.

Yatubidi tumwige na kufanya kama Mungu, yaani kuona chipukizi zuri la ngano ndani yangu, ndani ya wenzangu, kwa sababu kila mmoja ni ngano bora. Jambo jema tu katika mwingine linanipa ukweli juu ya mwingine, ni wema tu ndiyo unafumbua hali halisi ya mtu alivyo kwa sababu anatoka kwa Mungu. Uovu hauna uwezo wa kutufumbulia ukweli: Hakuna mtu anayefanana na uovu wake. Wewe hujaumbwa kwa mfano wa adui au wa giza, bali kwa sura ya Muumbaji aliye mwema.

Kwa hiyo kazi ya watu wa imani na ya watu wa dini ya kweli ni kukomaza mbegu bora ya imani, mapaji ya dhamira ya Mungu aliyoiweka ndani yetu. Binadamu wa kweli, siyo yule asiye na ndago au magugu, moyoni, au asiye na kasoro, bali ni yule ambaye anafunika uovu kwa wema; anatenda dhambi hata mara saba kwa siku lakini anafanya jema saba mara sabini.

Anafunika ubaya kwa wema; anaufifisha ubaya kwa upendo, kwa ukarimu, kwa nyimbo, kwa mwanga. Kwa hiyo kwanza tusishughulikie magugu, udhaifu au kasoro, bali tushughulikie kujenga na kukuza nguvu ambazo Mungu amezigawa kwetu, yaani nguvu za wema, ukarimu, uzuri. Ubaya hauwezi kukusaidia kulitenda jema unalotaka kulitenda. Ujumbe ni kwamba uheshimu, ujali maisha yaliyo ndani mwako, kwa kufanya hivyo uovu daima utashindwa na wema utashamiri.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.