2014-07-17 12:13:04

AMECEA: shuhudieni imani yenu kwa njia ya matendo!


Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Alhamisi asubuhi tarehe 17 Julai 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, yanayoongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo".

Katika Ibada ya Misa Takatifu, Kardinali Njue amesema kwamba, Bara la Afrika limekirimiwa kuwa na watu wenye uchaji wa Mungu. Yesu alimshinda Shetani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, lakini hadi leo, Shetani bado hajasilimu amri kwamba, alishindwa kwa goli la kisigino na anaendelea bado kuwasakama waamini na watu wenye mapenzi mema, ili kujiunga katika utawala wake.

Kardinali Njue amewapongeza Wamissionari waliojisadaka kwa ajili ya kuwatangazia watu wa Afrika Habari Njema ya Wokovu, changamoto kwa Wakristo kuendelea kuiboresha imani yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda wa maisha. Wazazi na walezi watambue dhamana na wajibu wao wa kuwarithisha watoto imani, maadili na utu wema. Waamini wajitaabishe kuishuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha adili.

Zaidi ya Maaskofu 200 kutoka katika Nchi za AMECEA wanashiriki katika mkutano wa kumi na nane wa AMECEA. Wamissionari wa kwanza walijitaabisha kutangaza Habari Njema ya Wokovu katika mazingira magumu kiasi kwamba, wengi wao walifariki dunia wakiwa na umri mdogo na hadi leo hii kuna makaburi yanayoonesha ushuhuda wa majitoleo yao, lengo lilikuwa ni kuwashirikisha wananchi wa Bara la Afrika imani na maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Wamissionari hawa walikuwa kweli waaminifu kwa Injili ya Kristo.

Kardinali Njue anawataka waamini Barani Afrika kusafisha dhamiri zao kwa kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake katika medani mbali mbali za maisha kwa kutambua kwamba, wasipokuwa makini na jasiri wanaweza kumezwa na malimwengu ambayo yanaendelea kulisakama Bara la Afrika. Rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu ni kati ya majanga ya kitaifa yanayoendelea kulisonga Bara la Afrika, kiasi cha kudhohofisha sera na mikakati ya kupambana na baa la umaskini, ujinga na maradhi Barani Afrika.

Maaskofu wa AMECEA wanasema, wanataka kuwahakikishia waamini wao kwamba, wanapania kuwahudumia kama wachungaji wema na watakatifu. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA unaoendelea mjini Lilongwe, Malawi.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu Askofu mkuu Tarcisius Ziyaye, Mwenyekiti wa AMECEA alikabidhiwa Pallio Takatifu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani, hapo tarehe 29 Juni 2014 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Askofu mkuu Ziyaye ni kati ya Maaskofu wakuu watatu ambao hawakubahatika kuhudhuria na kushiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu.

Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na waamini pamoja na viongozi wakuu wa Serikali ya Malawi na hasa wakati huu wanapoendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa Jubilee ya miaka 50 tangu walipojipatia uhuru wao. Sekretarieti ya AMECEA inawapongeza waamini na wananchi wa Malawi kwa ujumla wao kwa kufanikisha Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA. Serikali ya Malawi inashirikiana kwa karibu sana na Kanisa ili kufanikisha maadhimisho haya.







All the contents on this site are copyrighted ©.