2014-07-16 09:45:16

Tutaendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani Nchi Takatifu!


Monsinyo Liberio Andreatta, Mkurugenzi mkuu wa Idara ya hija ya Roma "Opera Romana Pellegrinaggi, ORP" pamoja na viongozi wenzake, Jumatatu tarehe 15 Julai 2014 wamendoka kuelekea Nchi Takatifu ili kusali pamoja na mahujaji walioko huko kwa ajili ya kuombea amani.

Taarifa zinasema kwamba, hija zinaendelea kama kawaida licha ya wasi wasi kuhusu usalama wa mahujaji kutokana na kinzani zilizopo kati ya Israeli na Palestina, hali ambayo imeifanya Jumuiya ya Kimataifa kulaani mashambulizi yanayofanywa na pande hizi mbili, kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wasiokuwa na hatia!

Idara ya hija inapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya kati kama alivyokumbushia Jumapili iliyopita wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana. Anasema, Sala inawasaidia waamini kutokatishwa tamaa na ubaya wala kushindwa na matumizi ya nguvu, chuki na uhasama; sala ni kikolezo cha majadiliano na upatanisho.

Ni changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kuwa kweli ni vyombo vya amani na upatanisho, hasa kwa wananchi wanaoishi katika Nchi Takatifu. Waisraeli na Wapalestina waonjeshwe mshikamano wa upendo, ili kuvunjilia mbali matumizi ya silaha ambayo yamekuwa ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu katika mchakato wa majadiliano, haki na amani!







All the contents on this site are copyrighted ©.