Mabalozi wapya wawasilisha hati zao za utambulisho, Ikulu, Jijini Dar Es Salaam
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania ameipongeza Ujerumani kwa kutwaa Kombe la Dunia
mwaka huu. Rais Kikwete ametoa pongezi hizo kwa Balozi mpya wa Shirikisho la Jamhuri
ya Ujerumani Mheshimiwa Egon Kochanke ambaye amewasilisha Hati zake za Utambulisho
Jumanne tarehe 15 Julai 2014 Ikulu, Jijini Dar Es Salaam.
“Naipongeza Ujerumani
kwa kuibuka washindi natumaini tutashirikiana vyema katika masuala ya utamaduni hasa
hasa katika kuinua kiwango cha soka nchini Tanzania na kuzisaidia klabu za Tanzania
kuanzisha shule maalum kwa ajili ya mpira wa miguu nchini.” Rais amesema na kuishukuru
Ujerumani kwa misaada mbalimbali katika sekta za Maji, Utalii, Usafiri wa majini na
maeneo mengine ya maendeleo.
Rais pia amepokea Hati za Mabalozi Richard Stuart
Man wa New Zealand na Bw. Claude Morel wa Ushelisheli ambao wana makazi yao Pretoria,
Afrika ya Kusini na Balozi Sander Kocsis wa Hungary mwenye makazi yake Jijini Nairobi
, Kenya.
Baadae mchana, Rais Kikwete amekabidhi Bendera ya Taifa kwa Timu
ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, inayotarajiwa kufanyika Glasgow kuanzia tarehe 23
Julai hadi tarehe 3 Agosti mwaka huu. Hafla ya kuiaga Timu hiyo imefanyika katika
Uwanja wa Taifa jijini na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Bernard Membe
na Naibu waziri, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia.
Timu
ya Tanzania inatarajiwa kuondoka kesho tarehe 16 Julai,2014 kuelekea Scotland ambapo
inatarajiwa kushiriki katika Riadha, Ngumi, Mpira wa Meza, Judo, Kuogelea, Baiskeli
na Kunyanyua vitu vizito. Rais amewaambia washiriki waende wakijua kuwa wana deni
la kutunza heshima binafsi kama wachezaji na heshima ya Nchi na Taifa kwa ujumla.
“Siri
ya mafanikio ni maandalizi mazuri na tumewekeza sana kwenye mafunzo na maandalizi
yenu na hivyo safari hii maandalizi yalikuwa mazuri, hivyo mna deni kubwa” Rais amesema.