Maaskofu wanawake! Kikwazo katika majadiliano ya kiekumene!
Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza linasema, kitendo cha Kanisa Anglikani kuridhia
wazo la kuwaweka wanawake wakfu ili kuwa Maaskofu ni kikwazo kikubwa katika mchakato
wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Kanisa Katoliki, kwa upande wake litaendeleza
mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwani hii ni sehemu ya mikakati yake ya kichungaji
na kwamba, litaendelea kushirikiana na Kanisa Anglikani kadiri inavyowezekana.
Hivi
karibuni, Sinodi ya Kanisa Anglikani iliyokutana tarehe 14 Julai 2014 huko New York,
imepitisha na kuridhia wazo la wanawake kuwekwa wakfu kuwa Maaskofu katika Kanisa
Anglikani. Dhana hii imekuwa ikifanyiwa kazi na Kanisa Anglikani kwa miaka mingi na
imekuwa ni chanzo cha migawanyiko ndani ya Kanisa Anglikani, kwa baadhi ya waamini
kutoafiki wanawake kuteuliwa na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Maaskofu wa Kanisa Anglikani.
Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox ndiyo bado ambayo
hayatoi nafasi kwa wanawake kuteuliwa na hatimaye kuwekwa wakfu kuwa Maaskofu. Kanisa
Katoliki limepiga hatua kumbwa katika majadiliano ya kiekumene tangu baada ya maadhimisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu,
changamoto kubwa iliyoko mbele ya Makanisa haya wanasema Maaskofu wa Uingereza ni
kuendelea kutolea ushuhuda makini wa Injili ya Kristo kwa watu wa nyakati hizi.
Wakati
huo huo, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni Dr. Olav Tveit amelipongeza
Kanisa Anglikani kwa kufanya maamuzi magumu ya kukubali na hatimaye kuridhia kwamba,
wanawake wanaweza kuteuliwa na kuwekwa wakfu kuwa Maaskofu. Hii ni "baraka kwa Kanisa
Anglikani". Katika nchi kama Amerika na Ustralia kuna Maaskofu wanawake tangu mwaka
1994, lakini nchini Uingereza wazo hili halikukubaliwa hadi mwaka huu, Sinodi ya Kanisa
Anglikani iliporidhia wazo hili.