2014-07-15 11:44:53

Umoja wa Mataifa unaipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon ameipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma kwa kusaidia kusitisha vita huko Senegal na kwamba, sasa amani inaanza kutawala tena. Hii ni sehemu ya mchakato wa kutafuta suluhu ya amani ya kudumu nchini Senegal baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa kipindi cha takribani miaka thelathini na miwili.

Kuanzia tarehe 28 Aprili 2014, mkuu wa Jeshi la waasi nchini Senegal aliwaamuru wanajeshi wake kusitisha mapigano, ili kuanza mchakato wa upatanisho, haki, amani na umoja wa kitaifa, kazi kubwa iliyoratibiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kwa kusaidiana na Serikali ya Marekani na wadau wengine wa kimataifa, anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Ni matumaini ya Jumuiya ya Kimataifa kwamba, mkataba wa kusitisha vita na mapigano nchini Senegal uliotiwa sahihi hapo tarehe 22 Februari 2014 utaheshimiwa na pande zote mbili, ili amani iweze kutawala tena kati ya watu. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaendelea kutekeleza mikakati yake ili kuhakikisha kwamba, amani ya kudumu inapatikana nchini Senegal.







All the contents on this site are copyrighted ©.