2014-07-15 11:25:30

Sera makini, majadiliano na ushirikiano ni mambo msingi katika kukabiliana na changamoto za wahamiaji!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kuanzia tarehe 14 hadi 15 Julai 2014 yuko nchini Mexico katika ziara ya kikazi, ili kushiriki katika semina inayolenga kuratibu tatizo la wahamiaji kati ya Serikali ya Mexico na Vatican. Akiwa nchini Mexico, Kardinali amekutana na mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka Honduras na Guatemala.

Akizungumza kwenye mkutano unaojaribu kuratibu hali ya wahamiaji kutoka Mexico, Kardinali Parolin anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa pamoja, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kujikita katika sera za mshikamano wa kidugu ili kukabiliana na changamoto ya uhamiaji kimataifa.

Sababu zinazopelekea makundi makubwa kuzikimbia nchi zao ni pamoja uvunjaji wa haki msingi za binadamu, vita, ukosefu wa amani na usalama, majanga asilia pamoja na ukosefu wa fursa za ajira. Watu wana matumaini ya kupata hali bora zaidi lakini matokeo yake wanakumbana na mkono wa chuma unaojionesha katika njaa, nyanyaso na dhuluma. Hawa ni watu wanaotumbukizwa kwa urahisi katika biashara haramu ya binadamu na wakati mwingine wanalazimishwa kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa ujira kiduchu, kwa wanawake na wasichana wanatumbukizwa katika utumwa mamboleo.

Kardinali Parolin anasema, Kanisa linaendelea kujielekeza katika kuwasaidia wahamiaji kwani linatambua na kuheshimu utu wa kila mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kundi hili linapaswa kuonjeshwa mshikamano wa upendo badala ya kuwatelekeza katika shida na mahangaiko yao ya ndani.

Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali anasema Kardinali Pietro Parolin, wanapaswa kushirikiana kwa ajili ya kutafuta na kuendeleza mafao ya wengi; utume unaoendelezwa na Kanisa, Mama na mtetezi wa ubinadamu. Serikali zinawajibu wa kulinda mipaka yake, lakini pia ziwasaidie wahamiaji kadiri ya sheria za kimataifa na wahamiaji kwa upande wao, wajitahidi kuheshimu na kutekeleza sheria za nchi husika. Hapa kuna haja ya kujenga na kuimarisha utamaduni wa ukarimu na Kanisa hapa litaendelea kutekeleza utume wake kwa wahamiaji na wageni ili kudumisha haki jamii.

Kardinali Parolin anasema Vatican inatekeleza dhamana yake katika uwanja wa kimataifa kwa kushirikiana na nchi mbali mbali, kwa kuwa ni mwanachama wa Mashirika ya Kimataifa pamoja na kuwa na wawakilishi wake katika nchi 118 duniani. Hizi ni juhudi zinazopaswa kutekelezwa kwa njia ya mshikamano kwani hakuna nchi inayoweza kujidai kwamba, ina rasilimali ya kutosha ili kukabiliana na tatizo la wahamiaji, lakini kwa njia ya mshikamano wa kitaifa na kimataifa, tatizo hili linaweza kukabiliwa kikamilifu. Sera makini, majadiliano na ushirikiano wa kimataifa ni mambo msingi katika kukabiliana na tatizo la wahamiaji duniani







All the contents on this site are copyrighted ©.