Sera na mikakati ya uchumi inayojali utu na heshima ya binadamu!
Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Vatican wamehitimisha
semina iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "kwa ajili ya uchumi shirikishi", changamoto
inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya
Furaha, "Evangelium gaudium". Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 12 Julai 2014
aliwatembelea na baadaye kupata pamoja nao chakula cha mchana.
Baba Mtakatifu
akizungumza na wajumbe hawa amegusia mwelekeo wa uchumi unaotoa kipaumbele cha kwanza
kwa binadamu na mahitaji yake msingi. Uchumi usijali utu na heshima ya binadamu, hapo
mwanadamu atanyanyasika na kudhulumiwa, huu ni uchumi usiojali wala kuguswa na mahangaiko
ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, binadamu anapaswa kuwa ni kiini cha mikakati
na sera za uchumi na maendeleo endelevu. Anawashukuru wajumbe wa mkutano huu kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake, ili kweli aweze kuheshimiwa na
kuthaminiwa.
Uchumi usiojali utu na heshima ya binadamu utakumbatia utamaduni
wa kifo na matokeo yake yanajionesha kwa idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa Barani
Ulaya. Wazee hawana nafasi tena katika mikakati na sera za kiuchumi kwani hawazalishi
tena, lakini hata vijana walio na umri chini ya miaka ishirini na mitano hawana fursa
za ajira wala hawana nafasi ya kujiendeleza na masomo. Ikiwa kama huu ndio mwelekeo
wa sera na mikakati ya kiuchumi, dunia inaelekea kubaya!
Kwa namna ya pekee,
Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe kwa kushiriki kikamilifu katika semina hii ili
kutoa mwelekeo wenye uwiano mzuri, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu
na heshima ya binadamu.