Msikate tamaa na kushindwa na ubaya! Endeleeni kusali!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala na tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili
tarehe 13 Julai 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili
ya kusali na kuombea amani katika Nchi Takatifu.
Bado anakumbuka lile tukio
la tarehe 8 Juni 2014 alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza,
Rais Peres wa Israeli pamoja na Rais Abbas wa Palestina ili kuombea amani Mashariki
ya Kati!
Baba Mtakatifu anasema kwamba, baadhi ya watu wanaweza kufikiri kwamba,
mkutano ule wa sala haukuwa na mafanikio yoyote, lakini hii si kweli, kwani Sala inawasaidia
waamini kutokatishwa tamaa na kushindwa na ubaya, wala matumizi ya nguvu kushika hatamu
badala ya majadiliano na upatanaisho. Baba Mtakatifu anawaalika wadau mbali mbali
kuongeza juhudi zao katika kukomesha uadui na chuki kati ya watu, ili amani na mafao
ya wengi yaweze kushika mkondo wake.
Baba Mtakatifu amewaongoza waamini na
watu wenye mapenzi mema waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu
Petro mjini Vatican kusali kwa ajili ya kuombea amani, ili Mwenyezi Mungu awaongoze
katika amani ya kweli, awajalie ujasiri wa kukataa kishawishi cha vita kwani kwa njia
ya vita kila kitu kinapotea, awakirimie ujasiri wa kuonesha kwa vitendo njia za ujenzi
wa amani pamoja na kuwawezesha kusikiliza kilio cha wananchi wao wanaotaka wabadilishe
silaha kuwa ni vyombo vya amani, wasi wasi na woga kuwa ni alama ya matumaini na kinzani,
kuwa ni kielelezo cha msamaha!
Baba Mtakatifu pia aliwakumbusha waamini kwamba,
Jumapili iliyopita Mama Kanisa ameadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani, kwa kuwataka
waamini kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya Mabaharia. Anawaalika wahudumu wa
maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea kuwasaidia mabaharia na kwamba, anawaweka
wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria nyota ya bahari.
Amewashukuru
viongozi wa Kanisa na waamini wa Familia ya Radio Maria waliokuwa wanafanya hija ya
maisha ya kiroho katika madhabahu ya Bikira Maria wa Jasna, Gòra, Czestochowa, Poland.
Anawashukuru kwa kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake.
Baba
Mtakatifu ametambua uwepo wa wanashirika wa Shirika la Mtakatifu Camillo wa Lellis,
wanaoadhimisha Jubilee ya miaka 400 tangu alipofariki dunia. Anawaalika wanashirika
hawa kuwa kweli ni alama ya Yesu Kristo, Msamaria mwema anayejinyenyekesha kwa ajili
ya kuwaganga majeraha ya mwili na roho kwa kuwapaka mafura ya faraja na divai ya matumaini.
Anawapongeza kwa huduma makini wanayotoa kwa ajili ya wagonjwa, waendeleze upendo
kwa wagonjwa.