Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!
Kwa mara nyingine tena tujumuike pamoja katika kuitafakari familia kama shule ya fadhila.
Kwa vipindi
hivi tutaanza kuitafakari fadhila ya unyenyekevu ambayo ndiyo msingi wa maelewano
mema na usitawi wa familia. Mara nyingi kukosa unyenyekevu kumekuwa ni chanzo cha
uvunjifu wa amani katika familia. Familia ikitawaliwa na unyenyekevu, hapo amani itajengwa
na itadumu.
Kristo Bwana, anatualika sisi sote tuwe wanyenyekevu akisema ”jifunzeni
kutoka kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini
mwenu”. (Mt. 11:29). Na pengine anatuasa akisema “Anayejikweza atashushwa, na yeyote
anayejushusha atakwezwa (Mt 23:12). Unyenyekevu ni ngazi ya kupanda juu, zaidi na
zaidi.
Unyenyekevu ni nini? Unyenyekevu ni hali ya moyo na akili inayomfanya
mtu ajikubali alivyo na awakubali wengine walivyo. Kwa njia ya unyenyekevu mtu anatambua
analopaswa kutenda na analitenda na pia asilopaswa kulitenda na halitendi. Kwa njia
ya unyenyekevu, mtu anawapa wengine nafasi ya kuwa wanavyotakiwa kuwa katika haki.
Kwa njia ya unyenyekevu, tunakomesha vilema vyetu vyote vya majivuno, kiburi, maringo,
kujionaona na kujikweza.
Fadhila ya unyenyekevu inachukuliwa kuwa ya msingi
na kiongozi wa fadhila nyingine zote. Mt. Augustino anaendelea kusema kuwa “Kimsingi
ni katika unyenyekevu mtu anafanywa kuwa mfuasi wa Kristo, na kwa hilo roho inaandaliwa
kuungana na Mungu.” Mambo yote ni lazima yapate msingi wake katika unyenyekevu. Unyenyekevu
unachukua nafasi ya kwanza kwa vile, unafukuza majivuno.
Fadhila ya unyenyekevu
inatudai kujishusha ili tuinuliwe. Inatufanya tujione si kitu ili tuonekane kuwa ni
kitu. Inatufanya tuwajali zaidi watu kuliko kujijali na kujipendelea sisi wenyewe.
Inatufanya tuoneshe upendo wetu zaidi kuliko kutaka kupendwa. Inatufanya tuwaheshimu
zaidi wenzetu kuliko kutaka kuheshimiwa.
Kwa njia ya unyenyekevu, tunaweza
kufundishwa, kuelekezwa, kuongozwa, kuonywa, kulindwa, kutetewa na kukuzwa kwa ujumla.
Ni fadhila ya msingi sana katika maisha ya mahusiano ya kila siku katika familia na
katika jumuiya yoyote ile ya watu. Hata marafiki wa kawaida tu, au wachumba wakikosa
unyenyekevu basi mahusiano yao daima hayatakosa malumbano, matusi, dharau, ukandamizaji
na kila aina ya mateso.
Pengine watu wengi hushindwa kuishi na sisi kwa sababu
tunakosa unyenyekevu, na ndio maana, hatuonyeki, haturekebishiki hatupendeki, hatuelekezeki,
hatufundishiki, daima tunajiona kuwa ndio wenye haki sana mbele za watu na mbele za
Mungu. Kukosa unyenyekevu kunatutenga na fadhila za Mungu. Tazama yule mfarisayo aliyekosa
unyenyekevu akajiona kuwa yeye ndiye mwenye haki sana. [Lk 18:9-14]
Familia
isiyojua unyenyekevu, ni uwanja wa vita daima. Vita za maneno na za mikono hazitakwisha.
Tangu mwanzo wa malezi watoto wafundishwe juu ya umuhimu wa unyenyekevu. Unyenyekevu
ni tendo la kijasiri kwa sababu linakudai kujishusha, kukomesha maringo, kiburi, kujikweza
na majivuno. Walio wanyenyekevu daima hupata kibali machoni pa Mungu. Neno linasema
“...Mungu huwapinga wajikwezao, bali huwapa neema wanyenyekevu” (Yak 4:6).
Wazazi
katika familia, wakinyenyekeana wao kwa wao hapo wanakuza zaidi upendo wao. Kiburi,
maringo, dharau na majivuno, hufukuza upendo. Lakini unyenyekevu hukuza na kudumisha
upendo. Inapotokea kwa sababu zozote wazazi wanaoneshana umwamba, hakuna anayetaka
kujishusha hata pale linapotokea kosa au kwazo la wazi, hapo upendo na furaha ya maisha
ya ndoa huingia katika dosari kubwa.
Ndoa nyingi zimeingia katika migogoro
ya kudumu sio kwa sababu ya matatizo makubwa, hasha! Pengine ni makosa madogomadogo
ya kawaida kabisa ya kibinadamu. Lakini kwa vile hakuna ile hali ya unyenyekevu, kuwa
tayari kujishusha, kila mtu anataka kujionesha yeye ni zaidi, na yupo sahihi zaidi
ya mwenzake; hapo ndipo mgogoro hukuzwa zaidi.
Hapa rai ya moja kwa moja tunaipeleka
kwa wanandoa! Wanandoa tukitaka amani, utulivu na maelewano ndani ya ndoa zetu, tuwe
wanyenyekevu. Tukomeshe vilema vya kiburi, dharau, kujiona na maringo. Unyenyekevu
ni daraja ya kufikiana na kuafikiana. Ukiwa mnyenyekevu, hata pale unapopatwa na tatizo,
mwenzi wako ni rahisi kukuelewa, kukupokea na kukuinua. Lakini ukikosa unyenyekevu,
utamfanya mwenzio ashangilie ukipatwa na mabaya.
Unyenyekevu, ni kiti cha
kutuweka katika mazungumzo yenye mwafaka daima. Bila unyenyekevu, kila neno utakalotamka
litakuwa na virusi vya fujo. Wazazi tukiwa wanyenyekevu, watoto wetu wataiga mwenendo
wetu wa unyenyekevu nao pia tutawafundisha unyenyekevu. Sisi wazazi ndio waalimu wa
maadili katika Kanisa la nyumbani, basi, na tujitahidi kuwa wanyenyekevu.
Na
mtume Paulo anaelekeza kuuambata unyenyekevu, kwani ndiyo njia ya kujenga usitawi.
Anasema “msifanye chochote kwa moyo wa fitina au majivuno ya bure; muwe na unyenyekevu
ninyi kwa ninyi, na kila mmoja amwone mwenzake kuwa bora kuliko yeye mwenyewe. Pasiwe
na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu, bali faida ya mwenzake” (Fil. 2:3-4).
Tunaahirisha
mada yetu kwa leo, hadi kipindi kijacho, kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni
mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.