Serikali ya Malawi imesema kwamba, itajitahidi kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama
wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA unaimarishwa zaidi,
ili kuwawezesha wajumbe kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa amani na utulivu. Hayo
yameelezwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi baada ya kufanya mkutano na viongozi
wa Serikali ya Malawi hivi karibuni.
Serikali ya Malawi imeonesha utayari wa
kulisaidia Kanisa katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa AMECEA unaofanyika nchini
humo, kama kielelezo cha upendo, mshikamano na ukarimu kutoka kwa wananchi wa Malawi
kwa ugeni mzito utakaokuwemo nchini humo kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 27 Julai 2014
huko Lilongwe.
Ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi umepata pia
fursa ya kukutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Malawi Bwana Saulos Chilima,
aliyehabarishwa kuhusu kamati mbali mbali zilizoundwa ili kurahisisha maadhimisho
ya AMECEA huko Malawi. Professa Peter Arthur Mutharika, Rais wa Malawi anafuatilia
tukio hili kwa ukaribu zaidi na anatarajiwa kuhudhuria katika Ibada ya ufunguzi wa
mkutano mkuu wa AMECEA hapo tarehe 17 Julai 2014 pamoja na kuwahutubia wajumbe wa
mkutano huo.