Viongozi wa kidini na mchakato wa maendeleo Barani Afrika
Zaidi ya viongozi 200 kutoka Barani Afrika waliokuwa wanakutana Kampala, Uganda hivi
karibuni wameamua kuvalia njuga ajenda za maendeleo baada ya mwaka 2015, ili kuhakikisha
kwamba, maamuzi yaliyofikiwa Jijini Kampala yanatekelezwa kwa ukamilifu. Viongozi
wa kidini walikuwa wanajadili kuhusu Mipango ya Maendeleo ya Millenia kwa Mwaka 2015
na baada ya hapo.
Viongozi wa kidini wameamua kuendeleza mchakato wa kudumisha
haki, amani na upatanisho Barani Afrika; majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja
na ushirikiano wa dhati miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali kama njia ya kupambana
na misimamo mikali ya kiimani, jambo ambalo kwa sasa ni tishio katika mchakato wa
haki, amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Bara la Afrika.
Viongozi wa kidini
wanataka kuhakikisha kwamba, wanawake, watoto, vijana na watu wenye ulemavu wanahusishwa
kikamilifu katika kupanga na kutekeleza mikakati ya maendeleo katika maeneo yao, bila
kuwasahau waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu Barani
Afrika.
Itakumbukwa kwamba, Umoja wa Mataifa baada ya kuweka Malengo ya Maendeleo
ya Millenia kuanzia Mwaka 2000 hadi mwaka 2015, ulipania kuhakikisha kwamba, nchi
changa duniani zinapambana na umaskini uliokithiri pamoja na baa la njaa.
Watoto
wapewe fursa ya kupata elimu ya msingi; kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na fursa sawa
kwa wanawake; kupunguza vifo vya watoto wachanga pamoja na upatikanaji wa huduma bora
zaidi kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga chini ya umri wa miaka mitano. Malengo
mengine ni kupambana na ugonjwa wa Ukimwi, Malaria pamoja na magonjwa mengine; kulinda
mazingira sanjari na kujenga mshikamano wa kimaendeleo.