Waamini wanahamasishwa kuwa na ari na mwamko mpya katika mchakato wa utume wa mabaharia,
kwa njia ya huduma makini, tafakari ya kina, uwajibikaji na uratibu mzuri wa shughuli
za kichungaji kwa mabaharia na wavuvi, wanaohatarisha maisha yao kila kukicha. Hili
ni ombi ambalo linatolewa na Waratibu wa Kanda katika Utume wa Bahari, baada ya kuhitimisha
Kongamano la Utume wa Bahari hivi karibuni mjini Vatican.
Kongamano
hili liliandaliwa na Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji
na watu wasiokuwa na makazi. Wajumbe wanasema, pamoja na changamoto mbali mbali wanazokabiliana
nazo, wanakumbana kwa kiasi kikubwa na ukata wa fedha ili kutekeleza mikakati ya shughuli
za kichungaji kwa ajili ya Mabaharia na wavuvi katika maeneo yao.
Bado hakuna
ushirikiano mkubwa kati ya Maaskofu na Wafanyakazi wa Utume wa Bahari: Kikanda, Kitaifa
na Kijimbo. Mawasiliano bado ni hafifu sana kiasi cha kugumisha utekelezaji wa mikakati
ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Mabaharia na wavuvi. Kuna mambo mengi ambayo
yanaweza kutekelezwa kwa ajili ya Utume wa Bahari, lakini rasilimali ni tatizo kubwa
kwa wakati huu.
Kumbe, wajumbe wanasema, kuna haja kwa Baraza kuteua baadhi
ya wajumbe watakaoshiriki katika kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili
ya kugharimia shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa Bahari, unaokabiliana na
changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia,
ambako utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani.
Pamoja na mapungufu haya,
lakini wajumbe wanasema, kuna mambo mengi ambayo, wanapenda kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha
Kanisa kutekeleza, hasa kwa kuwakirimia ujasiri wahudumu wa maisha ya kiroho kwa mabaharia
kutekeleza wajibu na dhamana yao hata katika mazingira magumu sehemu mbali mbali za
dunia. Kuna haja kwa Kanisa la Kiulimwengu kutoa msisitizo zaidi kwa ajili ya Utume
wa Bahari katika Kanisa la Kiulimwengu.
Wajumbe wameshauri utekelezaji wa maamuzi
yaliyofikiwa kwneye Kongamano la XXIII la Utume wa Bahari lililofanyika mjini Vatican,
kwa kutaka Utume wa Bahari kuwa ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya katika
ulimwengu wa mabaharia na wavuvi, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linatumia vyombo
vya mawasiliano ya kisasa pamoja na mitandao ya kijamii ili kuweza kuwatangazia Mabaharia
na wavuvi Injili ya Furaha. Kuna haja pia ya kuendelea kuboresha shughuli za uratibu
wa Utume wa Bahari, ili uweze kuzaa matunda bora zaidi katika ulimwengu wa utandawazi,
kwa kutumia rasilimali watu na fedha; weledi na utaalam kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa
na wadau mbali mbali katika Utume wa Bahari.
Mwelekeo huu, unaweza kuwa ni
chachu kwa Mabahari na wavuvi wenyewe kujisikia kuwa ni sehemu ya wadau wa Uinjilishaji
Mpya, kwa kuwapatia msaada wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Biblia na Mafundisho
Jamii ya Kanisa, kwani hivi ni vitabu vyenye utajiri mkubwa katika ushuhuda wa imani
tendaji.
Katika mapendekezo, wajumbe wanaliomba Baraza la Kipapa kuangalia
upya mchakato wa kuwateuwa Waratibu wa Kanda, Utume wa Bahari; kwa kufafanua kazi,
wajibu, dhamana na majukumu ya kila mhusika; kiasi cha rasilimali fedha na watu anachotakiwa
kuwa nacho sanjari na maboresho ya mahusiano kati ya Utume wa Bahari na Mabaraza ya
Maaskofu Mahalia. Wanalishukuru Baraza la Kipapa kwa ajili ya shughuli za kichungaji
kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kwa kuwapatia fursa ya kuweza kukutana,
kujadili na kufahamiana zaidi pamoja na kuangalia changamoto zinazojitokeza katika
utume wao, sehemu mbali mbali za dunia.
Wajumbe bado wanakumbuka changamoto
iliyotolewa kwao na Baba Mtakatifu Francisko, aliyewataka kuwa ni sauti ya mabaharia,
wavuvi na familia zao, kwa kujikita zaidi na zaidi katika huduma kwa mabaharia na
wavuvi. Wanashukuru pia kwa kupata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa kuzunguka kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyetangazwa
kuwa Mtakatifu hivi karibuni. Wajumbe wa Utume wa Bahari wanahamasishwa kutoka katika
bandari salama za maisha yao, ili kuwaendelea mabaharia na wavuvi ili kuweza kukabiliana
na changamoto katika ulimwengu wa mabaharia na wavuvi.