2014-07-12 10:33:18

Ratiba elekezi ya Mkutano mkuu wa 18 wa AMECEA


Wajumbe wa Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA wameanza kuwasili nchini Malawi tayari kushiriki katika mkutano huu ambao unafunguliwa rasmi hapo tarehe 16 Julai hadi tarehe 26 Julai 2014, huko Lilongwe, Malawi.

Wajumbe wataanza tukio hili kwa mafungo ya maisha ya kiroho yatakayoongozwa na Askofu Mengesteab Tesfamariam wa Jimbo Katoliki la Asmara nchini Eritrea. Umoja ndiyo mada itakayofanyiwa kazi hapo tarehe 16 Julai 2014. Wajumbe watapata nafasi ya kusali, kutafakari pamoja na kufanya toba.

Majira ya jioni, Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na Monsinyo Pius Rutechura, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Afrika Mashariki na Kati, CUEA wamepewa dhamana ya kuwasilisha moyo, mwono, utume na kiini cha tunu msingi zinazofumbatwa na AMECEA.

Kardinali John Njue, tarehe 17 Julai, 2014 majira ya asubuhi anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA, unaoongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo". Nia ya Misa hii ni Uinjilishaji, ili kueneza Injili ya Furaha kati ya watu wa AMECEA. Viongozi mbali mbali kutoka Malawi wanatarajiwa kutoa neno la "karibu" kwa wajumbe wa AMECEA.

Hii itakuwa ni fursa ya pekee kwa Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi kukutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano wa AMECEA, siku chache tu baada ya Malawi kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipojipatia uhuru wake. Askofu mkuu Tarcisius Zizaye, Mwenyekiti wa AMECEA atatoa hotuba ya ufunguzi.

Ratiba inaonesha kwamba, tarehe 18 Julai 2014: Tema ya siku ni shukrani kwa kazi za kimissionari na sala kwa ajili ya kuombea amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia ndilo lililopewa dhamana ya kuwahamasisha wajumbe wa AMECEA. Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya familia atawamegea wajumbe tafakari ya kina kuhusu Familia, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia.

Baadaye wajumbe wataendelea kujadili kuhusu Uinjilishaji wa awali na hali halisi ilivyo kwa sasa katika Nchi za AMECEA. Hii ni mada inayotazamiwa kuchambuliwa na Padre Benedict Ssettuma. Mazingira ya kitamaduni, kisiasa na kijamii ni tema itakayowasilishwa na Askofu Eduardo Hiiboro wa Jimbo Katoliki la Tombura-Yambio, Sudan ya Kusini.

Tarehe 19 Julai 2014, tema inayoongoza mkutano wa AMECEA ni Familia na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limepewa dhamana ya kuhamasisha wajumbe katika siku hii. Uinjilishaji mpya kama fursa inayowawezesha waamini kujikita katika wongofu na ushuhuda wa imani wa imani ya Kikristo kwa kukazia umuhimu wa Familia na Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni mada itakayopembuliwa na Professa Clement Majawa kutoka CUEA.

Umuhimu wa Seminari na nyumba za malezi katika kukuza ari ya Uinjilishaji Mpya ni mada itakayofanyiwa kazi na Askofu Charles Kasonde wa Jimbo la Solwezi, Zambia.

Jumapili tarehe 20 Julai 2014 wajumbe wa AMECEA wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia mbali mbali Jimboni Lilongwe. Jumatatu tarehe 21 Julai 2014: Vijana ndiyo mada itakayoongoza ajenda za siku na itahamasishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan na Sudan ya Kusini. Mada kuhusu huduma za maisha ya kiroho kwa taasisi za elimu ya juu katika kuendeleza Uinjilishaji mpya itachambuliwa na Askofu Martin Mtumbuka wa Jimbo Katoliki Karonga, Malawi. Athari za teknolojia ya dijitali na njia za mawasiliano ya jamii katika azma ya Uinjilishaji mpya unaofanywa na Mama Kanisa, itachambuliwa kwa kina na mapana na Askofu Bernadin Francis Mfumbusa kutoka Jimbo Katoliki la Kondoa, Tanzania.

Tarehe 22 Julai 2014 mada ya siku ni utamadunisho na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limepewa dhamana ya kuhamasisha siku hii. Mada kuhusu Liturujia na Uinjilishaji Mpya kama njia za Uinjilishaji itapembuliwa na Askofu James Maria Wainaina kutoka Jimbo Katoliki la Murang'a, Kenya. Hapa utakuwa ni mwisho wa sehemu ya kwanza ya Maadhimisho ya Mkutano wa kumi na nane wa AMECEA huko Lilongwe, Malawi.

Tarehe 23 Julai 2014, wajumbe wengine wataanza kurejea nchini mwao na Maaskofu watabaki ili kumalizia sehemu ya pili inayohusu huduma. Idara na taasisi ambazo ziko chini ya AMECEA zitawasilisha taarifa zake. Tarehe 24 Julai 2014 tema inayoongoza majadiliano ya siku ni mshikamano na ushirikiano wa kichungaji na Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia limepewa dhamana ya kuhamasisha siku hii. Wajumbe watapitia tena Katiba ya AMECEA na Sheria zake pamoja na Mikakati ya shughuli za kichungaji.

Tarehe 25 Julai 2014 ni siku itakayoongozwa na mada ya Uongozi na Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea litahamasisha siku hii. Maaskofu watapitia ujumbe kwa Familia ya Mungu katika Nchi za AMECEA pamoja na kutangaza mada itakayofanyiwa kazi na mkutano mkuu wa 19 wa AMECEA na baadaye uchaguzi.

Tarehe 26 Julai 2014 itaongozwa na mada ya ushuhuda itakayohamasishwa na Sekretarieti ya AMECEA na hapa Mwenyekiti Mpya wa AMECEA anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA huko Lilongwe, Malawi. AMECEA itatumia fursa hii kuwatangaza viongozi wapya watakaokuwa wamepewa dhamana katika Idara na Taasisi mbali mbali za AMECEA na hapa Ujumbe kwa Familia ya Mungu kutoka AMECEA utasomwa na hapo Maaskofu watakuwa huru kuanza kujipanga ili kurudi katika majimbo yao!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.