2014-07-11 09:47:57

Ujumbe kwa Siku ya Mabaharia kwa Mwaka 2014


Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari, inayoadhimishwa tarehe 13 Julai 2014 anasema kwamba, kutokana na hali pamoja na utume wao, mabaharia pamoja na wavuvi ni watu ambao hawaonekani mara nyingi machoni pa watu, lakini ni watu muhimu sana katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Kanisa linawaalika waamini katika maadhimisho haya kutowasahau mabaharia millioni 1. 2 kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Katika historia ya maisha ya mwanadamu, bahari imekuwa ni mahali ambapo: wasafiri, wavumbuzi na wafanyabiashara wamekutana. Bahari imekuwa ni uwanja wa vita, huu ukawa ni mwanzo wa kuzaliwa na kufutika kwa baadhi ya mataifa katika uso wa dunia. Wafanyabiashara wengi wanaikumbuka bahari kuwa ni mahali muafaka pa biashara, kwani sehemu kubwa ya bidhaa inatotumika duniani inapitia baharini, kazi murua kabisa inayotekelezwa na mabaharia.

Mama Kanisa anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina kwa kuthamini bidhaa mbali mbali wanazotumia katika maisha yao ya kila siku ambazo ni kazi ya mikono na jasho la mabaharia. Hili ni kundi ambali linakabiliana na changamoto mbali mbali kila siku ya maisha yao. Mabaharia ni sehemu ya utume wa Bahari unaotekelezwa na Mama Kanisa ili kuwaonjesha mabaharia huruma na upendo wa Mungu, ili hatimaye, hata wao waweze kuwa kweli ni wahudumu wa Injili, katika maeneo yao ya kazi.

Maisha ya mabaharia ni magumu na yanakabiliwa na hatari kila kukicha. Ni kundi ambalo ni rahisi kabisa kupoteza maisha kutokana na nguvu asilia. Taarifa inaonesha kwamba, zaidi ya mabaharia elfu moja walifariki dunia katika kipindi cha mwaka 2012 kutokana na majanga asilia au kwa kugongana. Bado wanakabiliwa na tatizo na uharamia baharini ambalo limeendelea kuwa sugu mwaka hadi mwaka; kunyimwa mishahara na wakati mwingine kutuhumiwa kwa makosa ya jinai na kuzuiliwa bandarini kwa muda mrefu.

Hili ni kundi ambalo linaishi katika hali ya upweke na wakati mwingi halina hata chembe ya mapumziko; ni watu wanaokabiliwa na upweke pamoja na kukosa muda wa kuwa na familia zao. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka tisini, Kanisa limeendelea kuwa bega kwa bega katika huduma za shughuli za kichungaji kwa mabaharia kwa njia ya kitengo chake cha Utume wa Bahari.

Kila mwaka kuna idadi kubwa ya mabaharia wanaoonjeshwa upendo na ukarimu katika vituo vya Bikira Maria nyota ya bahari, hapa wanapata nafasi ya kuwasiliana na familia zao pamoja na kupata huduma ya afya na maisha ya kiroho. Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum linasema kwamba, Utume wa Bahari imekuwa ni sauti inayowatetea mabaharia, kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwasaidia mabaharia kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa!







All the contents on this site are copyrighted ©.