2014-07-11 09:02:03

Malawi wako tayari kwa mkutano mkuu wa 18 wa AMECEA


Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA Padre Ferdinand Lugonzo katika mahojiano maalum na Shirika la Habari za Afrika, CANAA anasema kwamba, mkutano mkuu wa kumi na nane wa AMECEA unaoanza tarehe 16 hadi tarehe 26 Julai 2014 utawashirikisha zaidi ya Maaskofu Katoliki 150 kutoka katika nchi za AMECEA.

Mkutano huu utakuwa na sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza ni mkutano wa kawaida utakaojadili mada kuu saba ambazo zitawasilishwa kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu kadiri yalivyopangiwa. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni “Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo”. Sehemu ya pili itawahusu Maaskofu wenyewe, kwani hapa watakuwa na jukumu la kupokea taarifa kutoka katika taasisi mbali mbali zinazoongozwa na AMECEA pamoja na kuwapangia wahusika majukumu mapya ya uongozi.

Mkutano huu anasema Padre Lugonzo unatoa mwanya mpana kwa wajumbe kuweza kushirikishana uzoefu, mang’amuzi, ili hatimaye, waweze kuibua mbinu mkakati wa kichungaji utakaobainishwa wakati wa kutoa tamko la mwisho baada mkutano huu. Asubuhi wajumbe watasikiliza na jioni wajumbe watashirikishana na baadaye kuwasilisha mawazo ya vikundi.

Katika kipindi cha siku nne, wajumbe watajadili shughuli za awali za kimissionari: hali halisi na changamoto zilizoko. Mazingira ya kitamaduni, kisiasa na kijamii ambamo Kanisa linaendelea kutekeleza utume wake. Uinjilishaji kama fursa ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo kwa kukazia maisha ya familia na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Teknolojia ya digitali na njia za mawasiliano katika utume wa Uinjilishaji; Malezi katika nyumba za kitawa; umuhimu wa huduma za maisha ya kiroho na taasisi za elimu ya juu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya sanjari na Liturujia na utamadunisho kama njia za Uinjilishaji.

Hadi sasa maandalizi yote yamekamilika hata kama AMECEA haikufanikiwa kukusanya kiwango cha fedha ilichokuwa imejipangia kwa ajili ya kugharimia maadhimisho ya mkutano huu, lakini Kamati kuu inakiri kwamba, imepata msaada wa kutosha kutoka kwa Waamini na Wasamaria wema ndani na nje ya Malawi.

Itakumbukwa kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi lilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa AMECEA kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1979 na kurudia tena kuwa mwenyeji kunako mwak 1995. Mkutano mkuu wa Maaskofu wa AMECEA ni kipindi cha sala, tafakari, umoja na mshikamano kati ya Familia ya Mungu kutoka katika nchi za AMECEA.








All the contents on this site are copyrighted ©.