2014-07-10 12:10:13

Uteuzi: Jimbo la Kigoma Tanzania lapata Askofu mpya


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Padre Joseph P. Mlola , wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS) kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania. Kabla ya uteuzi mpya , alikuwa ni Gombera wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala, Tabora Tanzania.

Askofu Mteule Joseph P. Mlola, ALCP / OSS, alizaliwa Januari 9, 1966 Mashati Rombo, Moshi. Baada ya elimu ya msingi na sekondari, alijiunga na seminari ndogo ya Uru (Moshi), na baadaye kujiunga Shirika la Utume wa Yesu akiwa katika Seminari Kuu Kenya, ambako alichukua masomo ya falsafa. Na alikamilisha masomo ya Teolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala, Tabora.
Alipokea Daraja la Upadre Julai 12, 1997, chini ya maisha ya Jumuiya ya Mapadre wa Kazi ya Roho Mtakatifu "Opus Spiritus Sancti - ALCP / OSS". Baada ya Upadrisho alishika nyadhifa mbalimbali ifuatavyo :

1997-1999:Paroko Msaisizi wa Parokia ya Nairagie Enkare, Jimbo la Ngong, Kenya;
1999-2000: Makamu wa Ngombera katika nyumba ya malezi ya Roho Mtakatifu, Morogoro Tanzania
2000-2001: Paroko msaidizi Parokia ya Caliti, Avellino, Italia;
2001-2005: Alijiunga katika masomo ya juu ya shahada ya Uzamivu (udaktari), katika kanuni ya Teolojia, katika Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana.
2005-2011: Makamu Ngombera katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Charles Lwanga Segerea, Dar-es-Salaam Tanzania ;
tangu mwaka 2011 hadi uteuzi mpya, alikuwa Gombera wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala, Tabora Tanzania.

Jimbo la Kigoma, liliundwa mwaka 1953,chini ya Jimbo Kuu La Tabora. LIna eneo la kilomita mraba 45 066 kukiwa na idadi ya watu milioni 2, ambao kati yao 515 701 ni Wakatoliki. Kuna Parokia 22, , Mapadre 55 ( Mapadre wa Jimbo wakiwa 42 na Mapadre wa Mashirika 13 ), watawa ni 65 na Waseminaristi 19.
Jimbo la Kigoma, imekuwa wazi tangu Juni 27, 2012, kufuatia Askofu wake Protase Rugambwa, kuteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kumteuwa kuwa Askofu mkuu, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mshirika ya Kimissionari ya Kipapa mjini Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.