2014-07-10 12:06:10

Umaskini bado unaliandama Bara la Afrika!


Bara la Afrika limeendelea kucharuka katika maboresho ya miundo mbinu, elimu na afya, lakini taarifa kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni mia nne wanaoishi katika mazingira magumu na umaskini wa kutupwa, hasa katika nchi ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hii inaonesha kwamba, itakuwa vigumu kwa Jumuiya ya Kimataifa kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Tangu mwaka 1990 wananchi wengi Barani Afrika wanaendelea kuishi chini ya kiwango cha dolla moja ya Kimarekani kwa siku. Idadi hii imeongezeka kutoka watu millioni 290 katika kipindi cha mwaka 1990 hadi kufikia watu millioni 414 kwa sasa, kiasi kwamba, Bara la Afrika licha ya mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa na nchi mbali mbali, lakini idadi ya maskini inaongezeka.

Wachunguzi wa mambo ya uchumi na jamii wanasema kwamba, vita, kinzani za kijamii, kisiasa, kidini na kikabila ni kati ya mambo yanayoendelea kuwatumbukiza wananchi wengi wa Afrika katika umaskini wa hali na kipato! Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimepelekea nchi wahisani kupunguza misaada yake kwa Bara la Afrika, kiasi cha kukwamisha miradi mbali mbali iliyolenga maboresho katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Afrika.

Utapiamlo ni kati ya majanga yanayoendelea kuwaandama watoto wenye umri chini ya miaka mitano Barani Afrika. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya watoto millioni 58 ambao wanakabiliwa na utapiamlo wa kutisha, ikilinganishwa na watoto millioni 44 waliokuwepo katika kipindi cha mwaka 1990. Idadi ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa imeongezeka maradufu.

Licha ya mapungufu yote haya, lakini kuna matumaini makubwa katika sekta ya elimu ingawa bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Idadi ya watoto wanaopaswa kuanza shule ya msingi imeongezeka kutoka asilimia 60% hadi kufikia asilimia 78%. Kuna matumaini katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia katika mikakati yake kwenye sekta ya afya inayolenga kupunguza maambukizi ya Maleria, Ukimwi na Kifua kikuu kutokana na maboresho makubwa yanayotolewa kwenye sekta ya afya.







All the contents on this site are copyrighted ©.