2014-07-10 09:36:51

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa!


Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia watu wa dini mbali mbali kushindwa kufahamiana na hatimaye kuishi kwa amani, umoja na udugu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zisizo na tija wala mashiko kwa watu.

Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbali mbali kufahamiana. Hii ni kati ya changamoto zilizotolewa na Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini pamoja na ujumbe wake walipokuwa wanatembelea na kukutana na viongozi mbali mbali wa kidini nchini Indonesia, ambako kuna idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam.

Ujumbe wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, umekumbushia kwamba, majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa Uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani. Waamini wanaweza kujenga na kudumisha umoja, udugu na urafiki kwa kusaidiana katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Ujumbe wa Vatican nchini Indonesia umepokelewa kwa heshima na taadhima, huo ni ukarimu unaooneshwa na waamini wa dini ya Kiislam wanaoishi huko Indonesia katika ujumla wao. Majadiliano ya kidini kati ya Waislam na Wakristo nchini Indonesia yamejikita katika mang'amuzi na maisha ya kila siku, tofauti kabisa na hali inavyooneshwa na vyombo vya upashanaji habari. Ujumbe wa Vatican umepata nafasi ya kushuhudia na kubadilishana uzoefu na mang'amuzi katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na udugu kati ya watu.

Waamini wa dini ya Kiislam wanaofanya kazi katika taasisi za Kanisa Katoliki wanasema, wanaendelea kufurahia huduma yao na kwamba, wanajisikia wako nyumbani na wala hawajawahi kutengwa wala kunyanyaswa kwa misingi ya kidini. Kila mtu anaheshimiwa kama binadamu na kwamba, tofauti zao za kiimani ni utajiri mkubwa unaoweza kutumika kwa ajili ya kudumisha amani, upendo na mshikamano wa kidugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.