Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini Tanzania
kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Wananchi kuhakikisha kuwa ifikapo Mwezi Novemba
Mwaka huu, kila Shule ya Sekondari katika maeneo yao, ina maabara kwa ajili ya masomo
ya Sayansi.
Rais Kikwete amesema hayo Mkoani Tanga katika nyakati tofauti
Wilayani Kilindi na Lushoto ambapo yuko katika ziara ya kikazi Mkoani Tanga tangu
tarehe 8 Julai hadi tarehe 12 Julai,2014. "Nataka ifikapo Mwezi Novemba, Mwaka huu
vyumba vya maabara viwe vimekamilika, tulipeana miaka miwili, imetimia" Rais amesema
na kuongeza kuwa lazima tusahihishe makosa tuliyofanywa ya kutojenga maabara wakati
tunajenga shule za sekondari nchini kote.
Mwaka 2006, Serikali ilihamasisha
ujenzi wa Shule za Sekondari nchini kote na muitikio ni mzuri, lakini hakukuwa na
uhamasishaji wa kujenga maabara. “Tumeamua kushughulikia suala la maabara ili kuongeza
idadi ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi kote nchini." Rais amesisitiza. Rais amesema
ameridhika na upanuzi wa Elimu katika ngazi za Msingi na Sekondari kote nchini na
Serikali inaendelea na hatua ya kutatua changamoto za ubora wa Elimu, kuongeza Walimu,
kuongeza Vitabu, ujenzi wa Maabara na Nyumba za Walimu kote nchini.
Akihutubia
katika mkutano wa hadhara Wilayani Lushoto Rais ameahidi kuboresha na kushughulikia
suala la ujenzi wa barabara ya kwenda Bumbuli na zaidi kuhakikisha anaweka barabara
ya lami katika mji wa Lushoto na mji mdogo wa Bumbuli. Rais anaendelea na ziara Wilayani
Lushoto na Mkinga ambapo anaendelea kuzindua miradi na kukagua miradi ya maendeleo.