Dumisheni misingi ya ndoa na familia, epukeni "michepuko"
Wajumbe kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati,
AMECEA, walishiriki katika kongamano kuhusu changamoto zinazoikabilia familia katika
karne ya ishirini na moja mintarafu utandawazi katika mazingira ya Kiafrika.
Kongamano
hili ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili
ya familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba
2014. Wajumbe wanakiri kwamba, kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kujionesha katika
familia ya mwanadamu. Kongamano hili limefanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki
cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA na kwamba, wajumbe wamesisitizia umuhimu wa Vyuo
vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki kuanza
kuangalia uwezekano wa kutoa kozi maalum kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia.
Lengo
ni kuwajengea wanandoa pamoja na wanandoa watarajiwa uelewa mpana wa maisha haya tangu
awali, kuliko kusubiri mafunzo ya ndoa, wiki mbili kabla ya kufunga Ndoa Takatifu
ambayo ina dumu hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Kumbe, ni muhimu wanandoa wakajiaandaa
barabara na wala si kukurupuka tu, kwa sababu ya mambo mpito kama vile: fedha, cheo
au nafasi ya mtu! Hapa Waswahili wanasema, wakati mwingine, hapendwi mtu, ila pochi
tu!
Jamii inajengwa katika msingi wa ndoa ndiyo maana Kanisa linaendelea kusimama
kidete kulinda na kutetea misingi bora ya maisha ya ndoa na familia inayojengeka katika
upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi, kadiri ya mpango wa Mungu, yaani kuzaa na kuongezeka
ili wapate kuijaza dunia. Haitoshi tu kuzaa na kuondoka, kwani watoto wanahitaji matunzo
na malezi bora kutoka kwa wazazi wao.
Kumbe, wazazi wanapaswa kuwajibika barabara
katika malezi na makuzi ya watoto wao: kiroho na kimwili, ili hatimaye, waweze kuwa
na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika hija ya maisha
yao hapa duniani. Licha ya changamoto kubwa zinazoikabilia Familia ya binadamu, kuna
haja ya kupambanua mambo msingi yanayogusa utu na heshima ya binadamu na haya yanapaswa
kuvaliwa njuga, hadi kieleweke!
Mabingwa mbali mbali katika masuala ya ndoa
na familia wameshirikisha mang’amuzi na ufahamu wao, tayari kuona familia Barani Afrika
zinaendelea kujikita katika tunu bora za maisha badala ya kuiga mambo hata yale ambayo
kweli ni kinyume cha tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiafrika.
Pamoja
na mambo mengine, wajumbe pia wamepembua Waraka wa Papa Francisko, “Evangelii gaudium”
Injili ya Furaha kadiri ya mazingira ya Bara la Afrika. Wamekazia dhamana na wajibu
wa wazazi na walezi katika kuwafunda watoto, kwani Waswahili husema, samaki mkunje
angali mbichi, akikauka, hapo utapata shida.
Lakini, ikumbukwe kwamba, Kanisa
Barani Afrika lina dhamana ya malezi kwa watoto wake, kumbe, katekesi makini inahitajika
na majiundo endelevu ni muhimu kwa waamini walei ili kuwajengea uwezo wa kuyatakatifuza
malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Waamini na watu wote wenye mapenzi
mema wajitaabishe kusoma Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ambao kweli ni muhtasari
wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili pamoja na Sala. Waamini wakiifahamu vyema
Katekisimu na kuimwilisha katika maisha na vipaumbele vyao, kweli wanaweza kuwa ni
chachu na mwanga wa dunia katika mchakato wa kuyachachua malimwengu kwa njia ya ushuhuda
wa maisha.
Wajumbe wanasema, kuna uhusiano wa karibu kati ya Familia na Maendeleo
endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Familia nyingi zinakumbana na changamoto
nyingi za maisha ya kijamii na kiuchumi, kiasi kwamba, wakati mwingine zinabaki njia
panda. Njia za mawasiliano ya jamii zinaendelea kupewa nafasi ya pekee katika majiundo
ya maisha ya kifamilia.
Kwa upande wa Bara la Afrika, njia za mawasiliano
ya jamii ni upanga wenye makali kuwili mikononi mwa binadamu, zinaweza kusaidia familia,
lakini kama watu hawatakuwa makini, njia hizi na mitandao ya kijamii zinaweza kuwa
ndo mwanzo wa kukengeuka kwa familia nyingi.
Barani Afrika bado ndoa mchanganyiko
zinaendelea kushamiri kwani mapenzi ni chaguo la mtu. Hapa kuna haja ya kuwasaidia
Wakristo wanaofunga ndoa mchanganyiko katika kutekeleza majukumu ya malezi kwa watoto
wao, jambo ambalo kimsingi si rahisi sana kwa watu wengi, hasa ukizingatia mfumo dume
unaoendelea kutawala Barani Afrika.
Wajumbe wamekiri kwamba, kuna haja ya
kufanya uwiano mzuri kati ya kazi na maisha ya kifamilia. Kuna baadhi ya watu wamejikuta
wakizama kwenye kazi kiasi cha kudhoofisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
na matokeo yake, uaminifu, ukweli na udumifu vinawekwa rehani, hapa ni mwanzo wa kuchuma
majanga kama vile Ukimwi, Magomvi ndani ya nyumba na talaka!