Yatimia miaka 25 tangu alipouawa Askofu Pietro Colombus,Mogadishu
Julai 9, Kanisa limefanya kumbukumbu ya kupita miaka 25, tangu yalipofanyika mauaji
ya Askofu Pietro Salvatore Colombus, aliyekuwa Askofu wa Mogadishu Somalia, Mtawa
wa Shirika la Mtakatifu Francis, aliyetumikia Kanisa katika nchi za Afrika kwa miaka
42, na maisha yake kukatishwa kwa mtutu wa bunduki hapo Julai 9, 1989. Aliuawa kwa
kupigwa risasi iliyo penya moyo wake akiwa nje ya Kanisa Kuu la Mogadishu na wauaji
wasiojulikana.
Kwa ajili ya kumbukumbu hii, Askofu Giorgio Bertin, Askofu
wa Djibout, ambaye pia ni Msimamizi wa Kitume wa Mogadishu, Jumatano hii majira
ya jioni, ataongoza Ibada ya Misa, katika mji wake wa asili wa Carate Brianza, katika
Jimbo Kuu la Milan.
Hayati Askofu Colombus Mfranciscan, ambaye hakuachana
na joho lake la kifranciscan na tarawanda miguuni, anakumbukwa kwa unyenyekevu wake
wa kichungaji, upole na ukarimu. Aliuawa akiwa na umri wa miaka miaka 67, mauaji yanayo
endelea kuwa kitendawili hadi leo hii. Mazishi yake yalifanyika katika hali ya faragha
yakihudhuriwa na watu wachache tu, kutokana na hali ya usalama ilivyokuwa kwa wakati
huo. .
Kuna hisi za mauaji hayo, kuandaliwa na Waislamu wenye msimamo mkali,
ingawa hakuna aliyekwisha dai kuhusika . Kutokana na ukosefu wa Usalama Mogadishu,
mpaka sasa, hakuna Mjumbe wa Papa Mogadishu, ila kuna msimamizi wa Kitume Askofu
Giorgio Bertin, wa JImbo la Djibout, ambaye ameeleza kwamba, kwa jinsi ilivyo hata
kwa wakati huu, haiwezekani kufungua ofisi za kudumu za uwakilishi wa Jimbo la Papa
Mogadishu. Lakini ni wazi kwamba, tokea Djibout , wanaweza kufanya kazi za uwakilishi
na wana uhusiano mzuri na serikali ya somalia, ambayo mara kwa mara, hutamka wazi
wazi kwao kwamba, iwapo watajiondoa, serikali hiyo, itaishia kuwa kafara katika mikono
ya watu wachache wababe wa Kiislamu.
Na kwamba hata baada ya kupita kipindi
cha miaka 25 tangu kutokea mauaji ya Askofu Colombus, bado kuna mabadiliko kidogo
sana katika utulivu wa kitaifa. Mwaka hadi mwaka , ghasia za mauaji na machafuko
zinaendelea kuwepo zikifanywa na wababe wachache wa Kiislamu wanaotaka kuiamurisha
serikali kama wanavyopenda wao iwe.
Na hii ni sababu kubwa inayozuia Kanisa,
kutenda zaidi hata katika utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Somalia, hata
katika maeneo ya vijijini kwa , wakulima na wafugaji. Shughuli hizi zote za kiuchumi,
ni wazi zimesimama kutokana na ukosefu wa usalama na ukosefu wa taasisi za serikali.