Mashindano ya kombe la dunia kwa mwaka 2014 huko Brazil, ni tukio ambalo limevuta
hisia za watu wengi pamoja na kuonesha mshikamano wa dhati na timu pamoja na wachezaji
wenyewe. Watu wamerukaruka kwa furaha kama Kulungu, timu zao ziliposhinda; wamelia
na kuombolezwa pale walipochakazwa kwa mabao utadhani ni mpira wa pete!
Watu
wamekesha ili kufuatlia na kuangalia hatima ya kabumbu ilivyokuwa inatandazwa huko
Brazil, kwa hakika kuna mengi ya kuweza kujifunza katika kipindi chote cha mashindano
ya Kombe la Dunia kwa Mwaka 2014.
Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linawaalika
waamini kutafakari kwa kina baadhi ya tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kung'amua
umuhimu wa kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu kati ya waamini na Jamii katika
ujumla wake. Waamini wajenge na kuimarisha utamaduni wa kukutana ili kushirikishana
mang'amuzi mbali mbali ya maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Ari, moyo na ushabiki
ambao watu wameonesha kwa timu zao za kitaifa, unaoweza pia kuwasaidia waamini kujenga
uhusiano wa karibu na Yesu pamoja na kuipenda Injili, kiasi hata cha kuweza kuwa tayari
kuitolea ushuhuda makini katika uhalisia wa maisha!
Baraza la Maaskofu Katoliki
Chile linawataka waamini kujenga utamaduni wa kukutana ili kushirikisha tunu msingi
za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo
na Kanisa lake; ili kuonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Hapa jambo linalopewa
kipaumbele cha pekee ni umoja, upendo na mshikamano wa kidugu kama timu ya mpira pasi
na ubinafsi. Ni changamoto ya kuwaangalia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii.
Waamini wajifunze kujisadaka kwa ajili ya kushiriki katika maisha
na utume wa Kanisa katika utekelezaji wa mikakati ya kichungaji; waamini wajenge na
kuimarisha upendo na mshikamano wa dhati katika mambo msingi ya maisha; umoja na udugu
viwe ni nguzo kuu katika maisha na utume wa Kanisa.