2014-07-08 10:24:59

Tamko!


lLifuatalo ni Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa Bunge Maalum la Katiba nchini Tanzania lililotolewa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alipokuwa anazungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam.
TAMKO LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA
KWA BUNGE MAALUMU LA KATIBA (BMK)

UtanguliziKatika ujumbe wetu wa Kichungaji wa Pasaka 2014, sisi Maaskofu Katoliki Tanzania, tuliwaandikia barua watu wote wenye mapenzi mema kwa nchi yetu tukiwaalika kuchukulia maanani mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati huu tunawaalika Watanzania wote kwa pamoja, tuungane kuwakumbusha wale waliopewa dhamana ya kukamilisha Rasimu ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwajibika binafsi na katika maridhiano kutupatia Katiba maridhawa. Tunawaasa tukiwaombea dhamiri zao zipate maono mapya, waweze kubeba kiaminifu dhamana hiyo walio kabidhiwa.

Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,

Kwa moyo wa Sala na tafakari makini tulifuatilia mlivyojadiliana katika BMK kuanzia mwezi Februari hadi Aprili 2014. Katika siku sitini na saba (67), ninyi wateule wa Rais mpatao mia sita (600), mlijadiliana pasipo umoja, mkishambuliana kwa kauli kali kati yenu, mkikashifiana pasipo udhibiti wa uongozi mliojichagulia wenyewe kwa kanuni na sheria mlizojitungia. Mwenendo huo ulikuwa wa kusikitisha na kuchukiza katika mahali pale panapoheshimiwa na wote.

Tulitegemea majadiliano katika kuheshimiana hoja za kizalendo na kiungwana zitokanazo na mambo na masuala makuu yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba. Badala yake tulijionea mabishano makali na mpasuko uliosababisha upotoshaji wa nia iliyokusudiwa. Hatimaye hila na gilba zikateka kabisa jukumu adili la BMK.

Tukumbuke Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa uthubutu na ujasiri wa kipekee, alianzisha mchakato wa kuunda Katiba Mpya, na kisha aliridhia kwa kuipokea rasmi kwa furaha Rasimu ya II ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Ni lazima sasa tujiulize, nini kimetokea hadi kugeuza kabisa mwelekeo mzima wa mchakato wa Katiba kwa kuikejeli na kuishutumu vikali Rasimu hiyo katika wakati wa kipekee kabisa wa kihistoria wa uzinduzi wa BMK? Hata kusahau gharama kubwa ambayo ilibebwa na walipa kodi? Na sasa hali inaonyesha dhahiri jambo hili limeiingiza nchi kati ka mgogoro mkubwa unaoashiria hatari mbeleni.

Mwaliko kwa wahusika wote kuwa na utashi wa kisiasa

Kwa maoni yetu, tatizo hill kubwa ambalo limekuwa kikwazo kikubwa linaonyesha kukosekana utashi wa kisiasa na wahusika kutokuwa wakweli juu ya suala zima la Mchakato wa Katiba.

Tunawaomba wajumbe wa BMK kuwa wamoja na kufanya kazi yenu kwa mtazamo usioegemea siasa za vyama. Kuandika Katiba ni kazi iliyo ngazi ya juu zaidi ya siasa za vyama, na hivyo utashi wa kisiasa wa kuunda Katiba Mpya kwa kuzingatia Rasimu II utaweza kuridhiwa kwa kuzingatia msingi huu.

Kwa kadiri ya hali ya nchi yetu ziko sababu za kutosha za kutaka Katiba Mpya. Sababu hizi ni pamoja na ufisadi, wananchi kujisikia kukosa usalama, nchi kutokuwa na dira, tunu msingi n.k.

Ni kwa hiyo, tunawasihi kwa mara nyingine tena ninyi wajumbe wa BMK kurejea katika sehemu ya pill ya mjadala hapo mwezi Agosti mkiwa na moyo na mtazamo mpya. Tunawaomba achaneni kabisa na ubinafsi, uwe wa mtu mmoja mmoja, ama katika vikundi. Kwa kazi yenu tusaidieni sisi watanzania tuweze kujivunia kuwa na Taifa adilifu tukifanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya manufaa na ustawi wa wote. Kumbukeni BMK mnao wajibu wa kimaadili kwa nchi yenu na vile vile kwa namna mnavyotekeleza wajibu wenu mnaandika historia ya nchi yetu.
Wajibu wa Kimaadili
Kubeba dhamana ya kuandaa Katiba Mpya ni wajibu wa kimaadili kwenu. Tambueni kwamba Watanzania hawako tayari kurudi nyuma na kuendelea na maisha yanayoongozwa na Katiba ya 1977, kwa sababu licha ya mapungufu yake na ukiukwaji mkubwa ambao umekuwa ukifanyika, kufanya hivyo (kuendelea kuongozwa na Katiba ya 1977) kutaleta migogoro mikubwa yenye kuhatarisha vikali amani nchini.

Wajibu miiokabidhiwa ikiwa mtautimiza kwa dhamira njema, mtalijengea taifa letu msingi imara, uliosheheni tunu za kimaadili ambazo ni heshima katika utu wa mwanadamu, umoja, mshikamano na kujali manufaa na ustawi wa wote. Ni lazima matunda ya kazi yenu yawe ni kulipatia taifa dira inayowapa watu msukumo wa kujenga pamoja taifa Ienye watu wamoja na wanaojaliana kwa stahamala katika tofauti zao. Wajibu wenu huo ni Mtakatifu, na hivyo ni kosa kubwa mno kuusaliti kwa sababu ya ushindani katika medani za kisiasa au kujitafutia sifa mbele ya watu.

Jukumu la Kihistoria

Kwa matokeo yoyote yatakayotokana na kazi yenu katika BMK, Watanzania watawawajibisha. Ikiwa matokeo yatakuwa yenye kuleta mema, na kuimarisha amani na utulivu nchini, watu wote watawashukuru na kuwasifu. Lakini kama tunda la kazi yenu litakuwa ni Ienye kuingiza nchi katika matatizo zaidi, kuwataabisha wananchi na kukosa maelewano baina yao, basi watu watawahukumu na kuwawajibisha kwa kukosa umakini katika jukumu hili muhimu mlilokabidhiwa.

Kwa sasa tunahitaji Katiba itakayowezesha ushiriki kamili wa watu katika maamuzi ya vipaumbele vya maendeleo yao na ya Taifa. Ni Katiba shirikishi katika matumizi ya madaraka, iii yatumike kwa ajili ya kuhudumia wote, badala ya wachache. Tunahitaji Katiba ambayo inaruhusu utawala wa sheria, haki sawa kwa wote, manufaa na ustawi kwa wote na kuheshimu UTU wa kila mmoja. Ni Katiba iwezayo kuzuia matumizi mabaya ya madaraka na ufisadi. Hicho ndicho wananchi wanachokitarajia kutoka kwenu.
Yeyote anayedharau hitaji la Katiba mpya ama anayejaribu kupuuza na kuweka kando Rasimu II, huyo sio mwakilishi wa utashi wa watu. Mwisho wake historia itamhukumu vikali mtu huyo.

Wajumhe wa K, msiwaangushe watu wenu.

Hitimisho

Sisi Maaskofu Katoliki Tanzania tunawaahidi Sala zetu iii Mwenyezi Mungu awaangazie Nuru yake na kuwajalia nguvu ya kiMungu muweze kukamilisha kazi kwa mafanikio, kadiri ya matarajio ya watu wake wa Tanzania.

Tunawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea wajumbe hao wa Bunge Maalum la Katiba wajaliwe neema za Mungu.

Dar es Salaam 27.06.2 14










All the contents on this site are copyrighted ©.