Professa Arthur Peter Mutharika, Rais wa Malawi, Jumapili iliyopita amewaongoza wananchi
wa Malawi katika kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Malawi ilipojipatia
uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Katika kipindi hiki, Malawi imepata mafanikio makubwa
katika sekta ya elimu, afya pamoja na miundo mbinu. Hali ya maisha ya wananchi wa
Malawi imeboreka maradufu na kwamba, demokrasia imekuwa na kuongezeka, sasa Malawi
ni kisiwa cha amani Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Rais Mutharika katika
hotuba ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya uhuru wa Malawi iliyohudhuriwa na
viongozi mbali mbali kutoka katika Nchi za SADC. Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameipongeza
Malawi kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa na demokrasia pamoja na kuendeleza mchakato
wa mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Malawi.
Katika maadhimisho haya, Serikali ya Malawi imetoa msamaha kwa wafungwa
403 kama kielelezo cha kusherehekea Jubilee ambayo kimsingi ni alama ya shukrani kwa
Mwenyezi Mungu. Malawi imeendelea kufanya mageuzi ya viongozi wa Serikali kwa njia
ya demokrasia na hivyo kuwa ni kati ya nchi zinazodumisha amani Barani Afrika anasema
rais Athur Mutharika.