2014-07-07 15:12:02

Wajane wanateseka sana!


Askofu Oliver Dashe Doeme wa Jimbo Katoliki la Maiduguri, Nigeria anasema kwamba, mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria yanaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wajane zaidi ya elfu mbili ambao wanalazimika kutunza familia zao baada ya kuondokewa na waume zao katika mashambulizi mbali mbali yanayofanywa Kaskazini mwa Nigeria.

Askofu Doeme anasema kutokana na madhara yaliyosababishwa na mashambulizi ya mara kwa mara, Kanisa kwa sasa linaona kwamba, linawajibika kuwasaidia wajane hawa kuweza kustahimili kishindo cha ugumu wa maisha, kwa kuwaonjesha huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Maiduguri ni kitovu cha mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram, Kaskazini Mashariki wa Nigeria.

Jimbo Katoliki la Maiduguri limeanzisha mkakati wa kuwajengea uwezo wajane, kwa kuwawezesha kiuchumi ili kuanzisha biashara ndogo ndogo zitakazowasaidia kukabiliana na ukata wa maisha kwa wakati huu pamoja na kuzisaidia familia zao ambazo kwa sasa zinateseka sana kutokana na makazi yao kushambuliwa mara kwa mara, uharibifu wa mali pamoja na watu wasiokuwa na hatia kuendelea kupoteza maisha.

Wajane hawa wengi wao ni akina mama wa nyumbani kiasi kwamba, hawana uwezo wa kukabiliana na ukata wa maisha, kumbe, kuna haja kwa Wasamaria wema kujitokeza kuwasaidia ili kuweza kusonga mbele kwa imani na matumaini, licha ya vitendo vya kigaidi vinavyowakatisha tamaa kana kwamba, hakuna Serikali nchini Nigeria!







All the contents on this site are copyrighted ©.