2014-07-07 11:18:05

Adhabu ya kifo imepitwa na wakati!


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anawataka wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kuridhia itifaki inayopiga rufuku adhabu ya kifo, suala hili litakapokuwa linajadiliwa kwa mara nyingine tena kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwa siku za usoni. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumza na wawakilishi wa Italia kwenye Umoja wa Mataifa.

Italia ni kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo ziko mstari wa mbele katika kuhamasisha kufutwa kwa adhabu ya kifo. Azimio hili kwa mara ya kwanza liliwasilishwa kunako mwaka 2012 na kuungwa mkono na Mataifa 111. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, adhabu ya kifo kwa watu wanaoishi katika ulimwengu wa Karne ya 21, imepitwa na wakati.

Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kufutilia mbali ukatili na unyama wanaofanyiwa binadamu wakati wa utekelezaji wa adhabu ya kifo. Kwa upande wake Balozi wa Italia kwenye Umoja wa Mataifa Bwana Sebastiano Cardi anasema ulimwengu pasi na adhabu ya kifo haupaswi kuwa ni kitendo cha kikundi kidogo cha watu bali mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, iko siku dhamana hii itapaswa kutekelezwa na kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.