2014-07-06 08:00:39

Utajiri mkubwa unafumbatwa katika huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuzungumza na kusalimiana na wafungwa kutoka katika Gereza la Isernia, Jumamosi tarehe 5 Julai 2014 alikwenda moja kwa moja kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Isernia-Venafro ili kuzungumza na wananchi kwa ujumla. Anasema, hapa ni mahali ambapo wananchi wanakutana na Kanisa kuu ni mahali ambapo waamini wanakutana na Mwenyezi Mungu, ili kusikiliza Neno ili waweze kuishi kama raia na ndugu. RealAudioMP3

Papa Celestini wa tano kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi ni watu waliokuwa na mguso mkubwa kuhusiana na huruma ya Mungu kwani walitambua kwamba, huruma ya Mungu inaleta mageuzi duniani. Mtakatifu Francisko na watu wa nyakati zake walionja umaskini mkubwa wa watu wao, wakaonesha mshikamano wa upendo kwa kuwajali na kuwa karibu nao kama ilivyokuwa kwa Yesu aliyewaonea huruma watu waliokuwa wanateseka na kudhulumiwa; akawahurumia na kuwakabidhi kwa Baba yake wa mbinguni.

Lakini zaidi amewaachia ushuhuda wa kinabii na urithi wa maisha ya kidugu unaofumbatwa katika Injili ya Kristo. Watakatifu hawa waliguswa kwa namna ya ajabu na kuaamua kuwamegea jirani zao huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hii ndiyo zawadi kubwa kama Wakristo wanavyosali katika ile Sala kuu ya Baba yetu "Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe waliotukosea".

Hii ni sala inayoonesha dira na mwelekeo wa maisha unaofumbatwa katika huruma ya Mungu. hapa kuna huruma, rehema, maondoleo ya dhambi na uponywaji wa maisha ya kiroho. Ni unabii wa Nchi mpya unaoonesha usawa katika matumizi ya maliasili na kazi kila mtu akipata mahitaji yake msingi kwani mshikamano na ushirikiano ni vielelezo vya upendo wa kidugu. Watakatifu walionesha ushuhuda katika umaskini na huruma ya Mungu kwa kujisadaka wenyewe kwa ajili ya jirani zao.

Huu ndio mwelekeo mpya wa uraia katika kumbukumbu ya Mtakatifu Pietro del Morrone, Shemasi na Papa Celestin wa tano na uhalisia wa Jubilee ya Celestin ambayo Baba Mtakatifu ameizindua na tangu wakati huu, milango yote ya huruma ya Mungu imefunguliwa na kwamba, hapa si kukimbia matatizo ya ulimwengu bali ni jibu makini linalotolewa na Injili yaani, upendo kama nguvu inayosafisha dhamiri, nguvu inayopyaisha mahusiano ya kijamii, nguvu inayoweza kupanga na kutekeleza sera mbadala za kiuchumi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, kazi, familia badala ya uchu wa mali na faida kubwa!

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, huu si mwelekeo unaotumiwa na walimwengu na kwamba, kama waamini si watu wanaoot ndoto wala kuyaweka mawazo yao kwenye ombwe, bali njia inayowaelekeza watu katika haki na amani. Kama binadamu wanatambua kwamba, wao pia ni wadhambi, hivyo wanajiweka chini ya huruma ya Mungu inayowawezesha kupata matunda ya toba na wongofu wa ndani kazi ya huruma ya Mungu.

Wakati huo huo, Askofu Camillo Cibotti wa Jimbo Katoliki Isernia-Venafro anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kufika kati yao ili kuzindua Mwaka wa Jubilee ya Celestin, ili hata katika shida na changamoto wanazokabiliana nazo: kiuchumi, kijamii na kiroho waweze kuwa na matumaini kutoka kwa Kristo na Kanisa lake kwa kuweka mbinu mkakati wa kichungaji unaowashirikisha Watu wa Mungu kwa kuendelea kuthamini miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Anaombea familia Jimboni humo ili ziweze kuwa na ujasiri wa kusimama imara katika misingi ya imani, utu na maadili mema.

Rehema na neema zinazotolewa katika Jubilee ya Celestin ni alama ya upendo na mshikamano kwa Makanisa yanayoendelea kuteseka, ili waendelee kuwa kweli ni watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu bila kuchoka, Bikira Maria njia ya mwanga awasaidie katika mikakati yao ya kichungaji kwa kutetea zawadi ya maisha, kwa kujenga jamii inayojipambanua kwa haki, usawa na utakatifu wa maisha kwa kujikita katika kanuni na tunu msingi za maisha ya Kikristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.