2014-07-06 09:05:00

Jisadakeni kwa ajili ya Kristo na Jirani zenu!


Kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, ufukara na utii watawa wanawekwa wakfu kuwa ni mashahidi wa kinabii katika maisha na utume wa Kanisa. Ni watu wanaoweza kujisadaka na kuwa ni mfano na kielelezo cha kuigwa katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na utulivu sanjari na maendeleo endelevu ya binadamu.

Kwa njia ya maisha ya kijumuiya wanaonesha kwamba, inawezekana kabisa watu kuishi kama kaka na dada na kuunganika pamoja, licha ya tofauti zao msingi. Watawa wanapaswa kudhihirisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwamba, inawezekana watu wakaishi kwa pamoja na kupendana kidugu, huku wakiimarishwa kila siku katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sala za Kanisa.

Ni changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika, Africae Munus, kwa kuwataka watawa kuhakikisha kwamba, wanaendelea kumwilisha karama zao kwa ari ya kweli ya kitume katika maisha na utume wa Kanisa, huku wakijitahidi kumfuasa Kristo bila ya kujibakiza. Watawa wanachangamotishwa kuwa kweli waaminifu kwa karama za mashirika yao pamoja na kuendeleza ari na mwamko wa kimissionari sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.

Askofu mstaafu Mathias Isuja Josefu wa Jimbo Katoliki Dodoma, Jumamosi, tarehe 5 Julai 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya Masista wanne wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu waliokuwa wanaweka nadhiri zao za daima mbele ya Sr. Eufrasia Julius, Mama mkuu wa Shirika hili Kanda ya Tanzania. Askofu mstaafu Isuja amewataka watawa kuwa macho na makini na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, vinginevyo wanaweza kujikuta wanamezwa na malimwengu na hapo kutakuwa ni kilio na kusaga meno!

Askofu mstaafu Isuja amewakumbusha watawa kwamba, wanajisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao, dhamana wanayopaswa kuilinda na kuiendeleza kwa njia ya: Uaminifu na udumifu katika nadhiri; maisha ya sala na kijumuiya; msamaha na upendo kadiri ya kanuni na sheria za Shirika husika. Kwa njia ya nadhiri, watawa wanakuwa ni mali ya Mungu na Kanisa, tayari kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Watawa waoneshe moyo wa kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa, kufundisha shuleni pamoja na kutoa katekesi makini kwa familia ya Mungu, ili iweze kufahamu kwa kina: Imani, Sakramenti, Maisha adili na Maisha ya Sala ndani ya Kanisa.

Watawa wafanye yote haya bila ya kujibakiza, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Masista wa Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu wanachangamotishwa na Mama Kanisa kusoma alama za nyakati kwa kutoka kifua mbele ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha. Waoneshe ukarimu unaobubujika kutoka katika undani wa mioyo yao, tayari kuhushuhudia upendo wa Kristo kwa njia ya maisha yao matakatifu.

Ibada hii imehudhuriwa na Familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Dodoma, Watawa na ndugu na jamaa za Masista walioweka nadhiri zao za daima ambao ni: Sr. Rose Ngowa, Sr. Resituta Mrema, Sr, Beatrice Hilary na Sr. Rose Nyekobhe.







All the contents on this site are copyrighted ©.