2014-07-05 13:36:00

Wafanyakazi: zingatieni tafiti za kisayansi na majiundo makini ya kazi!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi asubuhi tarehe 5 Julai 2014 amewasili Mkoani Molise, Kusini mwa Italia na kupokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali, wakiongozwa na Askofu mkuu Giancarlo Bregantini wa Jimbo kuu la Campobasso-Boiano. RealAudioMP3

Baadaye, Papa amekwenda moja kwa moja kwenye Chuo Kikuu cha Campobasso na hapo amewahutubia wafanyakazi kutoka ndani na nje ya mkoa wa Molise kwa kukazia umuhimu wa tafiti za kisayansi na majiundo makini katika ulimwengu wa kazi, ili kujibu changamoto zinazojitokeza kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Anasema, mwenyezi Mungu anaendelea kumshangaza na kumchangamotisha mwanadamu kuwa na ujasiri wa kuvunjilia mbali vikwazo kwa kuonesha kipaji cha ugunduzi kielelezo cha matumaini.

Amewapongeza vijana wanaojizatiti katika kilimo ili kusaidia shughuli za uzalishaji kwa kutambua kwamba, si rahisi kupata majibu muafaka na wazi yanayojikita katika ugunduzi ili kutumia kikamilifu rasilimali inayopatikana katika eneo husika. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kweli ili ardhi iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Amewataka wakulima kutumia vyema ardhi waliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu kwani hii ni kati ya changamoto kubwa zinazomkabilia mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Ardhi itumike vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu kwa kuheshimu kazi ya uumbaji. Uharibifu wa mazingira una madhara makubwa sana kwa binadamu.

Changamoto nyingine inayojitokeza katika ulimwengu wa wafanyakazi ni wanawake wanapaswa kufanya kazi na wakati huo huo kutekeleza majukumu yao ya kifamilia. Huu ni ushuhuda wa kweli unaohitaji kuwa na uwiano mzuri kati ya wajibu wa kazi na dhamana ya kifamilia, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu katika sekta ya uchumi ambamo mwanadamu anaishi. Ni mwaliko kwa wazazi kutenga muda wa kutosha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia zao kwani maendeleo ya uchumi mamboleo hayana nafasi tena kwa familia, kwani inaonekana kana kwamba ni kupoteza muda.

Hapa kuna haja ya kuheshimu na kuthamini Jumapili, siku ya mapumziko si tu kwa ajili ya waamini bali kwa ajili ya wafanyakazi wote kwani hapa kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni kanuni maadili.

Jambo la msingi ni kuangalia mambo yale yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kuendeleza kazi msingi kwani kipaumbele cha kwanza hapa ni binadamu na wala si faida ya kiuchumi; mahusiano ya kifamilia na wala si ya kibiashara na kwa waamini ni kujitahidi kujenga mahusiano na Mwenyezi Mungu pamoja na Jumuiya ya Waamini.

Umefika wakati muafaka wa kujiuliza ikiwa kama kufanya kazi Jumapili ni kielelezo cha uhuru wa kweli! Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kielelezo cha uhuru wa kweli!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anasema anapenda kuungana na wafanyakazi na wafanyabiashara kuomba kuanzishwa kwa mchakato wa "mkataba wa kazi" kama njia ya kupambana na ukosefu wa fursa za ajira mkoani Molise, kwa kuunganisha nguvu za pamoja ili kuokoa nafasi za kazi kwa kuwa na mkakati makini kwa kushirikiana na viongozi wa kitaifa. Mkataba wa kazi unaoweza kusoma alama za nyakati kwa kuchangamkia fursa zinazotolewa na sera za kitaifa na kutoka katika Jumuiya ya Ulaya.

Baba Mtakatifu anawahimiza wafanyakazi kujizatiti katika mwelekeo huu, kwani kuna matumaini kwamba, unaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa hata kwa mikoa mingine pia. Utu na heshima ya binadamu; mahitaji yake msingi kwani inasikitisha kuona kwamba, mzazi anashindwa kutekeleza wajibu wake msingi kwa kuipatia familia yake chakula kwa vile hana fursa ya ajira. Jambo hili linasikitisha kwani linamwondolea mtu utu na heshima yake, kumbe, kuna haja ya kufanya kazi ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu!

Baba Mtakatifu anawashukuru wafanyakazi kwa kumzawadia Picha inayoonesha "Umama", kielelezo cha maisha na matumaini mapya. Anawashukuru kwa zawadi, lakini zaidi kwa ujumbe unaofumbatwa katika zawadi hii ambayo imesheheni kwa matumaini.

Kwa upande wake, Professa Gianmaria Palmieri, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Campobasso, kwa niaba ya wafanyakazi na wakulima kutoka mkoa wa Molise, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea, kwani hii ni sehemu ambayo imekiriwa utajiri mkubwa wa maliasili, utamaduni, mapokeo lakini zaidi kwa rasilimali watu, watu ambao ni waaminifu, wenye kiasi na wachapakazi, lakini kwa bahati mbaya wanaishi pembezoni mwa Jamii.

Hapa kuna changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza kwani vijana wengi wanajikuta hawana nafasi za ajira hivyo kuukimbia mkoa huu ili kujitafutia nafuu ya maisha. Ukosefu wa ajira ni tatizo kubwa mkoani hapo na kwamba, kuna wawekezaji na wafanyabiashara wamelazimika kufunga shughuli zao kutokana na ukata wa fedha.

Mkoa huu umebahatika kuwa na rasilimali nyingi, zikitumika kikamilifu zinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika ukuaji wa uchumi na maisha ya watu. Wafanyakazi wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatia moyo, ari na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha bila ya kukata tamaa.

Naye Gabrieli Maglieri kijana mwenye umri wa miaka 28 amemshirikisha Baba Mtakatifu Francisko jitihada zake katika masomo, ili kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo kwa kutunza na kuendeleza mazingira; kwa kuheshimu na kuthamini kazi inayotekelezwa na wakulima, changamoto kwa vijana kujihusisha na shughuli za kilimo badala ya kuwaachia wazee peke yao na kwamba haki inapaswa kutendeka!

Mama Eliza Piermarino, amemshirikisha Baba Mtakatifu changamoto anazokabiliana nazo katika maisha yake ya kazi na wajibu wake kama Mama wa familia nyumbani. Amezungumzia kuhusu ufanisi na changamoto kubwa anazokabiliana nazo katika ulimwengu wa kazi. Haya ni mang'amuzi yanayowagusa wanawake wengi wanaofanya kazi ofisini na viwandani. Ameonesha wasi wasi kwa maisha ya familia yake kwa siku za usoni kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kitaifa!









All the contents on this site are copyrighted ©.